Breaking

Saturday 16 December 2023

MIRADI YA BILIONI 48 KUIMARISHA UCHUMI WA VIWANDA PWANI


Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha wanasimamia vyema utekelezaji wa miradi ya maji Pangani, Kimbiji mpaka Chuo cha Uhasibu na Kwala kwa ufanisi ili iweze kuwa na tija kwa wananchi na kukuza uchumi wa viwanda kwa Mkoa wa Kibaha.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba ya utekelezaji wa miradi hiyo Mhe. Aweso amesema kuwa miradi hii ni tegemeo kubwa kwa wakazi wote pamoja na kukuza maendeleo ya Mkoa wa Pwani na maeneo ya Dar es Salaam Salaam Salaam, hivyo mkandarasi anatakiwa asimamiwe kwa ukaribu ili tija ya mradi ionekane kwa wananchi.

Mhe. Aweso ameeleza kuwa miradi hii ikikamilika pasiwepo na usumbufu katika kuunganisha wananchi kwenye huduma kwa kuwa ni haki ya kila mmoja, ni haki kwa mwananchi kupata huduma ya majisafi kwa wakati sambamba na wananchi kulipa bili sahihi za maji, lakini sio vyema kwa mwananchi kubambikizwa bili ya maji.

"Mwananchi anapaswa kushirikishwa kwa ukaribu kujua kiwango cha maji alichokitumia ili ajue bili anayopaswa kulipa, wasoma mita washirikishe wananchi wakati wa usomaji mita," ameeleza Mhe. Aweso.

Waziri Aweso ameitaka DAWASA kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwa kuanza kutumia mita za malipo ya kabla (prepaid meters) ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa malalamiko ya bili za maji.

"Huu ni wakati sahihi kwa Wizara ya Maji kuanza kutumia teknolojia hii ya mita za kulipa kabla kwa kuwa zitasaidia kuleta mageuzi nchini kwenye utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi," amesema Mhe. Aweso.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge amesema kuwa kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya majisafi Pwani, upatikanaji wa maji kwa Mkoa wa Pwani umefikia wastani wa asilimia 86 na juhudi zinaendelea za kuboresha huduma.

"Tunaridhishwa na jitihada za DAWASA ya uboreshaji wa huduma na tunaimani kwa kasi hii tutaweza kufikia asilimia 95 ya upatikanaji wa huduma kwa mwaka 2025," ameeleza Mhe. Kunenge.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA ndugu Kiula Kingu ameeleza kuwa jumla ya miradi mitatu ikiwemo mradi wa Kwala, Pangani na mradi wa Kimbiji mpaka Chuo cha Uhasibu imesainiwa kwa lengo la kuboresha huduma kwa Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.

Amesema kuwa miradi hii inatekelezwa kwa fedha za Serikali na DAWASA kwa bilioni 48, ambapo mradi wa maji Pangani utanufaisha wananchi 14,868 wa maeneo ya Kibaha - Msufini, Lulanzi, Tamco na Pangani.

Mradi wa maji Kimbiji mpaka Chuo cha Uhasibu unalenga kunufaisha wakazi wa Tazara, Ukonga mpaka Gongo la Mboto. Pamoja na mradi wa Kwala unaolenga kunufaisha wananchi 7,901 wa Bandari Kavu pamoja na vitongoji vya Kwala.




Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages