Breaking

Wednesday 7 February 2024

UJUMBE KUTOKA OFISI YA RAIS UMETEMBELEA TAASISI YA DIT KUJIFUNZA UUNDAJI WA MAGARI

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji imetembelea Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), kwa lengo la kujifunza na kupata maoni juu ya kuboresha na kukuza sekta ya uundaji magari nchini.

Ujumbe huo uliambatana na wadau kutoka sekta Mbalimbali ikiwemo wadau kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambapo ulipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Taasisi hiyo ikiwemo karakana ya kuongeza mfumo wa gesi asilia kwenye Magari (CNG) pamoja na kiwanda cha kutengeneza vipuri na Chombo cha Moto cha Gurudumu tatu.

Akizungumza na ugeni huo, Mkurugenzi wa Kampuni Tanzu ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT Comp Ltd) Dkt.John Msumba ameeleza kufurahishwa na ujio huo ambao umefika kuona kazi zinazofanywa na taasisi ambapo amesema kuwa DIT ina wajibu wa kuonesha kile kinachofanyika kwa kuwa haya yote yana nia ya dhati ya kutatua changamoto.

Hata hivyo amesema kuwa kampuni inapambana kuhakikisha kuwa inazalisha vyombo vinavyotumia umeme ikiwemo Chombo cha moto cha gurudumu tatu kwa wingi pamoja na kuwajengea wataalaam wao ujuzi mkubwa kwenye maeneo ya kuunganisha, kutafsiri pamoja na kuchora vyombo hivyo kwa ajili ya kuzalisha vyombo vyenye ubora mkubwa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages