Breaking

Saturday 30 March 2024

KAMANDA KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI TANGA AELEZWA MAFUNZO YANAYOTOLEWA NA AMEND KWA MADEREVA BODABODA

Na Mwandishi Wetu, Tanga

MKUU wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga William Mwamasika amesema mafunzo ya usalama barabarani yanayotolewa na Taasisi ya AMEND kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi kwa madereva bodaboda Jiji la Tanga yanakwenda kupunguza ajali kwa madereva hao.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Tanga Kamanda Mwamasika amesema taarifa alizonazo mpaka sasa madereva bodaboda 300 katika Jiji la Tanga wamepata mafunzo ya usalama barabara pamoja na huduma ya kwanza pindi inapotokea ajali.

Amesisitiza  kupitia mafunzo hayo wataelimisha kanuni na sheria za usalama barabara kwa lengo la kuwawezesha bodaboda kujilinda na ajali za barabarani.

"Kwa kushirikiana na AMEND tumejipanga kutoa mafunzo hayo katika Wilaya zote za Mkoa wa Tanga.Tunajua

bodaboda wakipatiwa mafunzo ya  usalama barabara ajali zitapungua kwa kiwango kikubwa katika Jiji letu na tumeanza kuona Sheria zikifuatwa na madereva bodaboda na hii ni kwa sababu wamepata mafunzo,"amesema.

Kamanda Mwamasika amesema kupitia mafunzo hayo itasaidia madereva hao kuzifahamu sheria za usalama barabarani na kuzitii hivyo kupunguza vitendo vya uvunjifu wa sheria ikiwemo kupakiza zaidi ya abiria mmoja 

Kwa upande wao baadhi ya madereva wa bodaboda waliopatiwa mafunzo wamesema mafunzo hayo yamewasaidia kuongeza uwelewa kuhusu matumizi sahihi ya Sheria za usalama barabarani sambamba na kuzingatia alama na hivyo kutii sheria bila shuruti.

Dereva bodaboda Ali Ramadhani amepongeza kutolewa kwa mafunzo na kwamba wanatamani kuona madereva wengi waliopatiwa mafunzo hayo kwani wao wameanza kuona faida yake.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages