Breaking

Wednesday 6 March 2024

MABORESHO RUVU CHINI MBIONI KUKAMILIKA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imesema kuwa kazi ya maboresho ya kuondoa tope kwenye Mtambo wa kuzalisha maji Ruvu Chini uliosababisha kupungua uzalishaji kwa asilimia 20 iko mbioni kukamilika.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Ndugu Kiula Kingu ameeleza kupitia vyombo vya habari kuwa uchafu kwenye maji umesababisha tope kwenye machujio ya maji na hivyo kuathiri ubora na usafi wa maji yanayozalishwa kwenda kwa watumiaji.

"Tuliona ni vyema kutenga muda wa saa 36 kusafisha machujio ya maji ili kuwezesha kupatikana kwa maji yaliyo masafi na yenye ubora kwa watumiaji, amesema na kuongeza kuwa kazi ya kuondoa tope kwenye chujio kubwa ilianza tangu siku ya Jumanne na inafanyika usiku na mchana," amesema Ndugu Kingu.

"Mpaka sasa kazi imefikia hatua nzuri na leo jumatano zoezi la kuondoa tope itakamilika na kuruhusu baadhi ya pampu kuwashwa na huduma kurejea kwenye hali yake," ameeleza.

Ndugu Kingu ameeleza kuwa baada ya kukamilika kwa kazi hii huduma ya maji itaimarika na maji yaliyopungua kwa asilimia yanapatikana kwa usafi.

Ametoa wito kwa wananchi wote wanaoharibu miundombinu ya maji hasa kipindi hiki cha mvua kuacha mara moja kwa kuwa uharibifu unasababisha gharama kubwa kwa Mamlaka ya kusafisha mtambo kila mwezi tofauti na awali ambapo mtambo ulikuwa ukisafishwa kila baada ya miezi sita.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages