Breaking

Wednesday 3 April 2024

Tanzania Yasisitiza Uhuru wa Biashara na Usalama wa Nchi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amesema Tanzania inaunga mkono harakati za kuwezesha usafirishaji wa bidhaa kwa huru na haraka mipakani kwa kuzingatia usalama wa Nchi ili kukuza uchumi wa kanda nzima na Barani Afrika.

Dkt. Abdallah ameyasema hayo Aprili 2, 2024, wakati akichangia mjadala wakati wa Kongamano la Usimamizi wa Mipaka katika Ufanyaji Biashara Mpakani linalofanyika Nairobi, Kenya kuanzia Aprili 2 -4, 2024 likijumuisha wajumbe kutoka Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudan Kusini, Somalia, Tanzania na Afrika Kusini .

Amebainisha kuwa Kongamano hilo linatarajiwa kufikia makubaliano muhimu kuhusu mtengamano wa biashara na biashara mipakani yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi katika kanda.

Aidha, Dkt. Abdallah amesisitiza kuwa ushirikiano wa kikanda na diplomasia ya kiuchumi ni muhimu na ni ahadi iliyotolewa na viongozi wa Tanzania na Kenya walipokutana jijini Dar es Salaam July 26, 2023. Viongozi hao walisisitiza umuhimu kukutana mara kwa mara ili kujadili na kutatua changamoto za biashara mipakani.

"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshmiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kufungua Nchi kupitia diplomasia ya uchumi ambayo msingi wake mkuu ni mtengamano wa biashara za kikanda na kimataifa". Amesisitiza Dkt Abdallah.

Akizungumza katika Kongamano hilo, amesisitiza kuwa Tanzania ni Baba wa Amani na mtetezi wa muda mrefu wa amani na usalama katika Kanda ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla huku ikiwa inajali masuala ya haki za binadamu na utu wa raia wake.

Naye Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala,alielezea juhudi za Tanzania katika kuboresha usimamizi wa mipaka kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuboresha ufanisi wa mipaka na ufanyaji biashara.

Aidha, Dkt Makakala alitaja mifumo inayotumiwa na Tanzania ikiwemo Mfumo wa Uhamiaji wa Kielektroniki ulioanzishwa mwaka 2018, Mfumo wa Usimamizi wa Mipakani kwa njia ya Mtandao unaowezesha kubadilishana data na mawasiliano kati ya vituo tofauti vya mipakani.

Vilevile amebainisha kuwa Tanzania inafanya kazi na nchi jirani katika kuhakikisha harakati nzuri ya watu na biashara katika mipaka ya pamoja kwa kujumuisha timu za pamoja za uhamiaji katika vituo vya vya huduma za pamoja za mipakani na kamati za kikanda zinazoshughulikia changamoto za pamoja.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages