Breaking

Saturday 20 April 2024

WATANZANIA TUWEKEZE KWENYE KINGA ILI KUPUNGUZA GHARAMA ZA MATIBABU - WAZIRI UMMY


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kuwekeza zaidi kwenye kinga na sio tiba ili kupunguza gharama za matibabu pamoja na kuepuka magonjwa Yasiyoambukiza ikiwemo Saratani kwa kufanya mazoezi na kuzingatia mtindo bora wa maisha. 

Waziri Ummy ametoa wito huo Aprili 20, 2024 baada ya matembezi yaliyofanyika kwa ajili ya harambee za kuchangia ujenzi wa Hospitali ya kina mama ya MEWATA - ‘Well Women Center (WWC) iliyopo Mbweni Jijini Dar Es Salaam. 

“Matembezi haya yanafanyika kwa ajili ya kuanzisha harambee za kuchangia ujenzi wa Hospitali ya kina mama ya MEWATA - WWC, kwakweli ni jambo la msingi kwa sababu litongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za wanawake na watoto nchini Tanzania”. Amesema Waziri Ummy 

Aidha, Waziri Ummy amesema kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC) za 2020, zinaonesha kuwa, tatizo la Saratani ya matiti na Saratani ya mlango wa kizazi nchini limekuwa likiongezeka mara kwa mara. 

“Katika kila watu 100,000 watu 10 hugundulika kuwa na ugonjwa  wa Saratani ya matiti na watu 25 kwa kila watu 100,000 hugundulika kuwa na ugonjwa wa Saratani ya mlango wa kizazi, tuwahi kupima na kutibu Saratani kwa kuwa tukiweza kuzigundua mapema zinazuilika”. Amesisitiza Waziri Ummy

Amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kuhakikisha huduma za kinga na matibabu ya Saratani zinapatikana nchini kote kwa kuongeza vituo vya uchunguzi na matibabu ya awali ya Saratani ya mlango wa kizazi  na matiti ili kuweza kufanya uchunguzi wa awali wa Saratani hizi kwa haraka. 

Pia, Waziri Ummy amesema Serikali itawaunga mkono MEWATA kufikia wanawake wote wa mjini na vijijini katika kupata elimu na huduma za Afya ili kupunguza tatizo la Saratani ya mlango wa kizazi pamoja na Saratani ya matiti. 

Aidha Waziri Ummy ametumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi kuwapeleka watoto wao kwenda kupata chanjo ya kuwakinga na Saratani ya mlango wa kizazi kwa kuwa chanjo hiyo ni salama na haina madhara yoyote. 

Kwa upande wake, Mbunge wa Mchinga Mhe. Salma Kikwete ambae pia ni mlezi wa MEWATA amesema Taasisi hiyo imefanya kampeni kadhaa katika Mikoa Kumi na Moja (11) hapa nchini ili kuelimisha wanawake na kuwafanyia uchunguzi wa awali wa Saratani ya matiti na Saratani ya mlango wa kizazi. 

“Kampeni hizi zilisaidia sana kuonesha hali halisi ilivyo juu ya ongezeko la magonjwa haya Yasiyoambukiza ikiwemo Saratani ya mlango wa kizazi na Saratani ya matiti”. Amesema Mhe. Salma

Nae Makamu wa Rais wa MEWATA Dkt. Mary Sando amesema nia ya mewata ni kukuza mshikamano na uhusiano, kuhimiza na kukuza utafiti na kuboresha afya kwa wanawake na watoto huku wakitetea mabadiliko ya sera katika sekta ya afya.

Dkt. Sando amesema Kauli mbiu ya matembezi haya ni tushirikiane kutoa kipaumbele kwa ajili ya afya ya wanawake na watoto kwa ustawi wa jamii, na lengo la matembezi hayo ni kuanzisha mchakato wa kuomba ufadhili kutoka kwa washirika tofauti na marafiki wa MEWATA utakaosaidia katika hatua za kutunisha mfuko wa ujenzi wa awamu ya kwanza ya Kituo hicho cha MEWATA.

“MEWATA inafuraha kualika watu wote kwenye sekta ya afya, wadau mbalimbai wa masuala ya afya pamoja na watanzania wote kwa ujumla kwenye matembezi haya ambayo yatafuatiwa na mkutano wa wanachama wa MEWATA na wadau mbalimbali,”. Amesema Dkt. Sando.

Amesema Kituo cha MEWATA cha Afya ya wanawake na watoto (MEWATA-WWC) kinatarajiwa kujengwa Mbweni – eneo la JKT, Dar es Salaam. Na kitafahamika kwa jina la MEWATA WWC

Aidha amesema Kituo hicho kinatazamiwa kuweka mazingira salama na ya starehe ambapo wanawake kutoka kote Tanzania wataweza kupokea huduma kamili za afya, elimu ya afya na usaidizi unaoendana na mahitaji yao mahususi.

Pamoja na hayo amesema MEWATA itaungana na wafanyakazi wenzako na marafiki kutoka WHO kujumuika katika tukio hilo, wakitarajia uwepo wa Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya (MoH), Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tukio hili litahusisha Wajumbe ambapo tunatarajia uwepo wa Mhe. Dr. Dorothy Gwajima, Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Vikundi Maalum atakuwepo ili kutoa Mada kuu” Amesema.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages