Breaking

Friday 3 May 2024

TBS Yawataka Wafanyabiashara wa Vipodozi Kusajili bidhaa hizo

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wafanyabishara wa bidhaa za vipodozi kuhakikisha wanasajili bidhaa zao , kuthibitisha ubora wake pamoja na kusajili maeneo yanayohusika na uzalishaji, uuzaji na uhifadhi kwa mujibu wa matakwa ya sheria ya viwango Sura ya 130 ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.

Wito huo umetolewa leo Mei 3, 2024 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya wakati akifungua Kikao baina ya TBS na wazalishaji, waagizaji na wasambazaji wa bidhaa za vipodozi nchini.

"Madhara ya kiafya yanayoweza kusababishwa na matumizi ya vipodozi vyenye viambata sumu ni pamoja na saratani ya ngozi, kuathiri mfumo wa uzazi, kuathiri figo, kuathiri afya ya ngozi na kusababisha ngozi kushindwa kuhimili joto pamoja na kushambuliwa kirahisi na magonjwa ya ngozi". Amesema Dkt. Ngenya.

Aidha Dkt. Ngenya amesema katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023 hadi mwezi Aprili 2024, wamekamata na kuharibu vipodozi vyenye viambata sumu vinavyokadiriwa kuwa na uzito wa tani 114 na thamani ya shilingi bilioni 1.49.

Amesema kuwa Shirika litaendelea kuchukua hatua stahiki za kisheria kwa wale watakaoendelea kukiuka matakwa ya sheria katika uuzaji wa vipodozi.

Amesema wafanyabiashara hao wa vipodozi wanapaswa kuhakikisha wanazalisha na kusambaza bidhaa za vipodozi vilivyokidhi matakwa vya viwango ili visiweze kusababisha madhara ya kiafya kwa watumiaji wa bidhaa hizo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages