Breaking

Sunday, 16 June 2024

MAJI CUP YAANZA KUUNGURUMA KANDA YA ZIWA

  

Ligi ya Maji CUP inayoendeshwa na Taasisi ya watoa huduma za Maji nchini (ATAWAS) imeanza kuchezwa mkoani Shinyanga, ikishirikisha Timu kutoka Mamlaka za Maji Kanda ya Ziwa, ikiwa na lengo la kutoa ujumbe kwa wananchi juu ya kutunza vyanzo vya Maji,kuzuia upotevu wa Maji pamoja na kutunza Miundombinu ya Maji.


Ligi hiyo imeanza kutimua vumbi leo Juni 16,2024 ambayo itahitimishwa kesho katika Uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga ,ikishirikisha Timu kutoka Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA),Maswa (MAUWASA),Mwanhuzi na (KASHWASA)huku wenyeji wakiwa ni SHUWASA.


Mkurugenzi wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola, akizungumza wakati akimkaribisha Mtendaji Mkuu wa ATAWAS, amesema lengo la ligi hiyo ni kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya kutunza vyanzo vya Maji,kudhibiti upotevu wa Maji na kutunza miundombinu ya Maji.


Mtendaji Mkuu wa ATAWAS Costantino Chiwaligo, amesema huu ni mwaka wa nne sasa wakiandaa Ligi hiyo ya Maji Cup ambayo hufanyika kila mwaka kwa kushirikisha Kanda 10, na baada ya hapo Timu 32 ambao zitaibuka washindi kikanda watakwenda kucheza kitaifa Jijini Dodoma ili apatikane mshindi wa Jumla.


Amesema Ligi hiyo ya Maji Cup ni wazo ambalo lilitolewa na Waziri wa Maji Jumaa Aweso mwaka 2021 ikiwa ni sehemu ya Kampeni kwa ajili ya kufikisha ujumbe kwa wananchi kupitia michezo kutunza vyanzo vya maji,kuzuia upotevu wa maji, na kutunza miundombinu ya maji.

Amesema vyanzo vya maji visipotunzwa, ikiwamo miundombinu ya maji pamoja na maji kupotea ni hasara kwa wananchi, kwa sababu watakosa huduma ya maji na hata kusababisha mgawo.


“Kampeni hizi ni kuizindua jamii kuwa maji yakipotea ni shida kwao sababu watakosa huduma ya maji, hivyo ni vyema wakavitunza vyanzo vya maji, kuzuia upotevu wa maji pamoja na kuacha wizi wa maji sababu takwimu zinaonyesha upotevu wa Maji asilimia 40 husababishwa na Wizi wa Maji, ikiwamo kujiuganishia kinyemela na kuchepusha maji,”amesema Chiwaligo.


Aidha, amesema taasisi hiyo pia wapo kwenye hatua za kuanzisha Mita za Malipo ya Kabla ili kuzuia upotevu wa Maji, na kwamba zoezi hilo litaanzia Mkoa wa Shinyanga.


Naye Mgeni Rasmi Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko, akizungumza kwenye ufunguzi huo wa Ligi ya Maji Cup, ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kwamba waepuke kufanya shughuli za kijamii kwenye vyanzo vya maji, ili visijepotea sababu bila maji hakuna maendeleo.


Amesisitiza pia pale mwananchi atakapoona mtu akiiba Maji kwa kujiunganishia kinyemela kinyume na sheria watoe taarifa kwa Mamlaka husika, na hata wakiona kuna Mivujo ya Maji vivyo hivyo watoe taarifa ili kuzuia upotevu wa maji, huku akiipongeza SHUWASA kwa kujitahidi kuzuia upotevu huo wa maji kwa asilimia 17.


Kauli Mbiu katika Ligi hiyo ya ATAWAS Maji Cup 2024, inasema "Thamani ya Maji kwa Uhai na Maendeleo" huku Michezo ambayo inachezwa na Mpira wa Miguu pamoja na Pete, ambapo Shuwasa katika ufunguzi huo wamewafunga Mauwasa 4-1.


Maandamano ya kuingia katika uwanja wa CCM Kambarage.


Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoani Shinyanga (SHUWASA) Mhandisi Yusuph Katopola akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo.
Mtendaji Mkuu Taasisi ya watoa huduma za Maji Nchini (ATAWAS) Constantino Chiwango akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo.
Mstahiki Meya Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akizungumza wakati wa wazinduzi wa mashindano hayo.
Mstahiki Meya Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akizungumza wakati wa wazinduzi wa mashindano hayo.

Mstahiki Meya Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akikagua moja ya timu ya mpira wa miguu itakayokwenda kushiriki kwenye mashindano hayo.
Mstahiki Meya Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akikagua moja ya timu ya mpira wa miguu itakayokwenda kushiriki kwenye mashindano hayo.
Mstahiki Meya Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akikagua moja ya timu ya mpira wa pete itakayokwenda kushiriki kwenye mashindano hayo.




Mstahiki Meya Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko akipiga mkwaju wa penati kuashiria mashindano hayo yamezinduliwa rasmi.

Mstahiki Meya Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko (kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoani Shinyanga (SHUWASA) Mhandisi Yusuph Katopola. 





Baadhi ya Mashabiki waliojitokeza kwenye uzinduzi wa ligi hiyo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages