Na Happiness Shayo -Dodoma
Tanzania imeweka rekodi kubwa ya Kimataifa kwa miezi ya Januari hadi Machi 2024 kwa kushika nafasi ya 5 kwa nchi ambayo imeweza kuvutia watalii zaidi duniani na nafasi ya kwanza Barani Afrika kwa kuvutia watalii kimataifa, kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism).
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Angellah Kairuki (Mb) alipokuwa akichangia mjadala wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa fedha 2024/2025 na Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 leo Juni 26,2024 Bungeni jijini Dodoma.
Amesema pia Tanzania imeshika nafasi ya 4 kwa takwimu za January mpaka Machi, 2024 katika nchi zilizoongeza mapato yanayotokana na shughuli za utalii duniani na kushika nafasi ya kwanza Barani Afrika.
“Kwa takwimu za Benki ya Dunia za mwezi Mei, 2024 Tanzania imefanikiwa kupata Dola Bilioni 5.75” amesisitiza Waziri Kairuki na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kukuza na kutangaza utalii.
Amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia tangu aingie madarakani kwa upande wa kuvutia watalii kutoka nje ya nchi, Tanzania imefanikiwa kuongeza watalii kwa zaidi ya asilimia 96% ambapo hadi kufikia mwezi Desemba, 2023 watalii wa nje walikuwa takribani milioni 1.8 na watalii wa ndani kiwango kiliongezeka hadi kufikia asilimia 152% ambapo watalii takribani milioni 1.9 walifika hadi mwezi Desemba 2023.
Aidha, amesema kutokana na jitihada za Rais Samia Tanzania imeweza kutambulika Kimataifa ambapo kupitia takwimu za Shirika la Utalii Duniani kwa mwaka 2023 Tanzania ilishika nafasi ya 12 duniani kwa kuwa na ongezeko la idadi ya watalii wa Kimataifa kabla ya janga la UVIKO 19.
Katika hatua nyingine Waziri Kairuki ameipongeza Serikali kwa namna ambavyo Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2024/2025 imeendelea kuakisi umuhimu wa kuendelea kukuza Uchumi na kuweka mkazo katika kuweka mazingira bora ya uwekezaji na biashara, kukuza ajira, kukamilisha miradi ya Maendeleo ya kimkakati na kwamba kati ya Sekta chache zilizopewa kipaumbele Sekta ya Utalii pia imeonekana.