
Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila
Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila, leo Mei 27, 2025 ametoa somo zito kwa wanazuoni na wadau wa sekta binafsi kuhusu mwenendo wa deni la taifa la Tanzania na dunia kwa ujumla.
Kafulila ameshusha nondo kwa kutumia takwimu ambazo zinaonyesha kuwa wakati deni la dunia limekuwa likiongezeka, deni la taifa la Tanzania limebaki kuwa himilivu.
"Uchumi wa dunia wote unaendeshwa kwa mikopo, kwa maana ya kuwa ni debt financed," Kafulila alisema kwenye kongamano la wazi lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo.
Kongamano hilo limeandaliwa na PPPC kwa kushirikiana na Taasisi ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET) chini ya Mwenyekiti wake Prof. Rwekaza Mukandala.
"Kuna mjadala kuwa deni la taifa linaongezeka. Ni kweli deni linakua, lakini hii ni trend (mwenendo) ya dunia nzima," alisema.
"Changamoto ya Covid-19 iliathiri global supply chain (mnyororo wa ugavi duniani) na kutengeneza uhitaji wa kukopa zaidi kwa kuwa mahitaji ya nchi mbalimbali yanazidi kuongezeka kuliko mapato ya serikali kupitia kodi na mikopo yanavyoweza kumudu."
Kafulila amesema kuwa ongezeko la mahitaji ya rasilimali za kugharamia bajeti ya serikali yamefanya dhana ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kugharamia miradi ya maendeleo kuwa na umuhimu wa kipekee nchini Tanzania.
"Utekelezaji wa miradi ya PPP utapunguza presha kwenye bajeti ya serikali na kuhakikisha kuwa nchi inafikia mahitaji ya wananchi," alisisitiza.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa uchambuzi huru wa kitaalamu kutoka kwa wachumi wa taasisi mbalimbali zinazoheshimika duniani unaonyesha kuwa deni la taifa la Tanzania bado ni himilivu kulinganisha na nchi zote za Afrika Mashariki.
"Pamoja na kusema kuwa deni la taifa la Tanzania limekuwa linaongezeka, bado uchumi wetu ni himilivu kulinganisha na mwenendo wa uchumi wa nchi nyingi Afrika na duniani," alisema.
Kafulila, ambaye hupenda kuthibitisha hoja zake kwa takwimu, alitoa takwimu mbalimbali za uwiano wa deni na uchumi (debt-to-GDP ratio) ambazo zinaonyesha kuwa Tanzania bado tuko vizuri.
"Kwa Tanzania, uwiano wa deni kwa uchumi ni asilimia 47, ambayo ni ndogo kuliko nchi zote za Afrika Mashariki na nchi nyingi za Afrika kusini mwa janga la Sahara," aliongeza.
Kafulila ametoa takwimu zifuatazo kusisitiza hoja yake.
Mwenendo wa uwiano wa deni kwa uchumi:
🔘Duniani (wastani) 90%
🔘 Afrika (wastani) 67%
🔘 Ghana 90%
🔘 Malawi 84%
🔘 Rwanda 71%
🔘 Kenya 70%
🔘 Tanzania 47%