TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) imepanga kufanya mafunzo ya kukuza uwezo kwa wakuza mitaala na walimu nchini kwa kutumia Akili Mnemba (AI) ili kukuza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji.
Hayo yamebainishwa leo Mei 9, 2025 Jijini Dar es Salaam, wakati TET wakisaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitatu na Taasisi ya Tanzania AI Community kwa lengo la kuingiza matumizi ya AI katika ufundishaji na ujifunzaji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt. Aneth Komba amesema jukumu lao kubwa itakuwa ni kuhakikisha kwamba wadau hao wa teknolojia wanapata karikulam, silabasi na vitabu ili waweze kuwasaidia kuweza kutumia AI katika ufundishaji na ujifunzaji.
"Haya ni mapinduzi makubwa kwa hatua zinazoendelea kupigwa, kwa sasa duniani kuna maendeleo makubwa sana katika sayansi na teknolojia, kwahiyo matumizi ya AI katika ufundishaji na ujifunzaji yatampunguzia sana mzigo mwalimu," amesema Dkt. Aneth
Amesema lengo lao ni kuhakikisha kwamba wanawafiki walimu wote nchini wanaoweza kutumia teknolojia hiyo katika jirahisisha ufundishaji na ujifunzaji, na kwamba katika mtaa mpya wataingiza kipengele cha kutumia AI katika ifundishaji na ujifinzaji.
Aidha Dkt. Aneth ameishukuru Taasisi ya Tanzania AI Community kwa kuwa tayari kushirikiana na TET, hivyo wapo tayari kutimiza majukumu yao kama TET kuhakikisha wanaendana na teknolojia iliyopo kwa sasa/
Naye, Mkurugenzi wa Tanzania AI Community, Essa Mohamedal, amesema wamefurahi kushirikiana na Taasisi ya Elimu kwakuwa wataweza kuwaongezea uwezo walimu wote nchini na kuwafanya watekeleze vizuri zaidi majukumu yao.