Na OR- TAMISEMI
KATIBU Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa, Profesa Riziki Shemdoe amesema kwa sasa halmashauri zimepunguza utegemezi wa fedha kutoka Serikali Kuu kwa wastani wa asilimia 15.
Hatua hii imetokena na utekelezaji wa awamu ya tano ya programu ya maboresho ya usimamizi fedha za umma ambao unatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na kufikia tamati yake Juni mwaka huu.
Profesa Shemdoe ameyasema hayo jana wakati akiongoza kikoa cha Kamati Tendaji ya utekelezaji wa programu ya maboresho ya usimamizi wa fedha za umma (PFMRP) ambayo ilikuwa ikitekeleza katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Amesema ukusanyaji wa mapato umeongezeka jambo ambalo limepunguza utegemezi kutoka asilimia 8 mwaka 2016/17 hadi kufikia wastani wa asilimia 15.
" Ukiangalia kwa sasa utegemezi umekuwa ni wastani wa asilimia 85 ingawa bado ni mkubwa lakini tumepiga hatua, hata hivyo kwa upande wa majiji na baadhi ya manispaa utegemezi umepungua sana mfano halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam zinaweza kujitengemea kwa wastani wa asilimia 23 na kwa sasa hazipelekewi fedha za Uendeshaji wa Ofisi (OC) kutoka Serikali Kuu."
Profesa Shemdoe pia amesema matumizi ya fedha nje ya bajeti kwa halmashauri nchini umepungua kutoka asilimia 10 mwaka 2016/17 hadi kufikia asilimia 2 mwaka 2020/21.
Aliongeza kuwa upelekaji wa fedha zilizotengwa kwenye bajeti kutoka Serikali Kuu kwenda Mamlaka ya Serikali za Mitaa yameongezeka kutoka asilimia 60 mwaka 2016/17 hadi kufikia asilimia 85 mwaka 2020/21.
Profesa Shemdoe amesema kumekuwapo na kupungua kwa hoja za ukaguzi sambamba na kuongezeka kwa uwazi kwenye manunuzi.
Aidha, Profesa Shemdoe alisema mkakati uliopo ni kuzungumza na wadau kuangalia namna ya kuja na programu hii awamu ya sita ambapo mambo kadhaa yataingizwa ikiwamo ya kukabiliana na changamoto ya matumizi ya fedha mbichi.
" Pia tunataka programu ijayo iweze kusaidia kwenye kuongezeka kwa vyanzo vya mapato ili kuondokana na hali ya sasa ya kupandisha kwenye chanzo hicho hicho badala ya kuwa na vyanzo vingi ambavyo havitaumiza wananchi."
Kwa upande wa mratibu wa programu hiyo, Lucas Mrema alisema programu hiyo imeweza kusaidia kuimarisha mfumo funganishi wa usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha ambao umefungwa katika halmashauri 185.
Lengo la programu hiyo ni kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Aidha, wadau wa maendeleo wanaofadhili programu hiyo walibainisha kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana kumekuwapo na changamoto ya uhaba wa watumishi katika wa Idara ya Fedha na manunuzi jamba ambalo linafanya halmashauri zisifanye vizuri kwenye usimamizi wa fedha.
Pia kutokuwepo na usimamizi madhubuti wa sheria ndogo ambazo kama zingesimamiwa ipasavyo ukusanyaji wa mapato unheongezeka kwenye halmashauri.
Pia kutokuwepo na usimamizi madhubuti wa sheria ndogo ambazo kama zingesimamiwa ipasavyo ukusanyaji wa mapato unheongezeka kwenye halmashauri.