SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatarajia kuanzisha mfumo shirikishi wa tafiti za elimu ili kuboresha ufundishaji, ujifunzaji, na usimamizi wa takwimu ambao utarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wadau wa elimu.
Akizungumza leo Mei 14,2025 Jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano kati ya Bodi ya Mikopo ya Elimu Juu (HELSB) na tasisi ya Adapt IT (Adapt IT and HESL Technology Symposium), Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema lengo kuu ni kuwezesha matokeo ya tafiti zinazofanyika kuwa na tija katika kuimarisha sekta ya elimu kwa wadau wote.
Profesa Mkenda amesema tayari kamati ya wataalamu ilioundwa yenye jukumu la kupitia mifumo iliyopo na kuandaa mapendekezo ya uboreshaji, ipo hatua za mwisho za kukamilisha mapendekezo ya ujenzi wa mfumo wa takwimu wa sekta ya elimu.
Aidha amesema kuwa mfumo huo utawezesha upatikanaji wa takwimu zote za sekta ya elimu kupitia mfumo mmoja.
Ameeleza kuwa mfumo huo utakuwa na uwezo wa kupokea takwimu mbalimbali zinazohusiana na elimu kutoka katika mifumo mingine ya Serikali ikiwemo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Idara ya Uhamiaji na Ofisi ya Rais Tamisemi.
Pamoja na hayo amesema wizara hiyo inajipanga kuanza kutoa ripoti ya Mwaka ya Takwimu za Elimu (Basic Education Statistics Tanzania) inayohusisha taarifa za ngazi zote za Elimu na takwimu za shule na Vyuo Binafsi.
"Kumekuwa na malalamiko ya wadau wa elimu kwa muda mrefu kuhusu upatikanaji wa takwimu katika baadhi ya ngazi za sekta ya elimu kama vile vyuo vikuu, lakini ujio wa mfumo utakaowezesha kupatikana takwimu za elimu sehemu moja ni hatua muhimu". Amesema Profesa Mkenda.
Hata hivyo Waziri Mkenda amesema katika sekta ya elimu mfumo huo unakwenda kuwatambua wanafunzi wote na namba na zao hatua itakayosaidia kutambua kila hatua anayopitia mwanafunzi na wale wanaoshindwa kuendelea na masomo.
“Kupitia mfumo mzuri tutamtambua kila mwanafunzi kwa umri na kila hatua anayofikia. Hata vyuo vikuu tunataka tuwe na uwezo wa kujua idadi ya wanafunzi kwenye programu fulani na ni wangapi wanadondoka ili kutambua sababu,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) Dkt. Bill Kiwia, amesema kuwa kupitia Kongamano hilo wataangalia namna ADAPT IT ambao wana uzoefu wa teknolojia ya kutosha wamekumbana na changamoto zipi.
Amesema lengo la kuja na mifumo hiyo ni kusaidia upatikanaji wa huduma bora kwa wanafunzi na kupunguza gharama kwa Serikali.
“HESLB tumekuwa tukijenga mifumo yetu ya ndani kwa kutumia wataalamu wetu wa ndani maana hili ndilo lengo la serikali la kutaka mifumo isomane. Katika sekata ya elimu pia mifumo yetu inaenda kusomana kutokana na hatua zinazochukuliwa,” amesema