Breaking

Friday 25 March 2022

DIAMOND PLATNUMZ AIPONGEZA SERIKALI YA RAIS SAMIA KUWAUNGANISHA WASANII,KUREJESHA TUZO

 



Mkurugenzi Mkuu wa Wasafi Media na  Msanii maarufu ndani na nje ya Bara la Afrika, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platinumz amemshukuru  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuwaunganisha  wasanii ili sekta ya Sanaa iweze kuwanufaisha.


Diamond amesema haya leo Ijumaa Machi 25, 2022 mbele ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa alipotembelea  Kampuni ya Wasafi inayomiliki rebo ya Wasafi, Wasafi TV na Wasafi FM redio kwa lengo la kukagua  kazi za Sanaa.


Amesema Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni imefanya mapinduzi makubwa  katika sanaa kwa  kubuni mikakati mbalimbali ya kuwaunganisha na kuwanufaisha wasanii.



Miongoni mwa mikakati ameitaja mizuri ya Serikali kuwa ni pamoja na  kurejesha tuzo za muziki.


Kwa  upande wake Waziri  Mchengerwa amesema Serikali imeshatenga  fedha nyingi kwa ajili ya kuwekeza kwenye Sanaa ili wasanii waweze kunufaika.


"Nimekuja hapa leo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yangu  ya kukutana na wadau wa sekta ninazozisimamia  ili kuwaunganisha na Serikali yao, nimefurahi kuona wasafi mnaibua vipaji na kutoa ajira kwa wasanii nchini" amepongeza Mhe Mchengerwa



Amesema  Serikali itaendelea kuwasaidia wasanii wote bila kuwabagua na kwamba Serikali inathamini mchango mkubwa unaotolewa na wasanii nchini.


Akielezea kuhusu utoaji wa burudani wa vituo vyake Diamond amefafanu kuwa vinajitahidi kwenda na teknolojia ya kisasa katika kuendesha vipindi  vyenye maudhui ya kuelimisha na kuburudisha jamii.


Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri amepata fursa ya kutembelea na kukagua shughuli za kampuni hiyo na kujionea uandaaji wa vipindi mbalimbali vya michezo na burudani vinavyotangazwa na vituo hivyo.


Mkurugenzi wa vipindi wa Wasafi  Nelson Kisanga amesema  Wasafi FM imekuwa na vipindi maarufu vya michezo vya Sports Arena na Sports  court ambavyo vimekuwa na wasikilizaji wengi.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages