Breaking

Saturday 19 March 2022

KAMPUNI YA BARRICK YAKABIDHI MASHINE MBILI ZA KUPIMIA UVIKO -19 HOSPITALI YA MANISPAA YA KAHAMA

Afisa Afya wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Dkt. Said Kudra akimwelezea Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (kulia) kuhusu Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya shilingi Milioni 115 zilizotolewa na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema (katikati) akikata utepe wakati Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick Gold Corporation ikikabidhi Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga. Kulia ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare, kushoto ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Buzwagi, Rebecca Stephen.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare (kulia) akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya Shilingi Milioni 115 katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga leo Jumamosi Machi 19,2022. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema. Katikati aliyevaa kofia ni Meneja Mkuu wa Barrick Buzwagi, Rebecca Stephen
.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (kulia) akizungumza wakati Kampuni ya Barrick ikikabidhi Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya shilingi Milioni 115 katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga. Kushoto ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare akifuatiwa na Afisa Afya wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Dkt. Said Kudra.

************
Na Kadama Malunde - Kahama

Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Barrick Gold Corporation kupitia Migodi yake ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi imekabidhi Mashine (RT- PCR Machine) mbili za kupimia UVIKO- 19 zenye thamani ya Dola 50,000 sawa na shilingi za Kitanzania 115,000,000/= katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga.


Mashine hizo zimekabidhiwa leo Jumamosi Machi 19,2022 na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Buzwagi, Rebecca Stephen kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema kwenye hafla fupi iliyofanyika katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama.


Akizungumza wakati wa kukabidhi Mashine za Kupimia COVID – 19, Meneja Mkuu wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare amesema Mashine hizo zitasaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na hivyo kuwezesha utambuzi UVIKO – 19 kwa haraka zaidi.


“Kampuni ya Barrick kupitia Migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi inaendelea kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya UVIKO -19. Tunakabidhi mashine hizi mbili za kisasa za kupimia UVIKO – 19 ambapo kila mashine ina gharama ya Dola 25,000”,amesema Sangare.


Naye Afisa Afya wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Dkt. Said Kudra amesema mashine hizo zina uwezo wa kupima Sampuli nne ndani ya saa moja hivyo kuwahamasisha wananchi kufika katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama kupima afya zao ili kubaini kama wana maambukizi ya UVIKO- 19 .


Akipokea Mashine hizo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema ameishukuru Kampuni ya Barrick ameishukuru kwa kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya UVIKO – 19.


“Barrick hamjawa nyuma,mmekuwa kimbilio letu kila wakati, serikali inapokuwa na jambo,mmekuwa mkifungua mikono yenu. Asanteni sana kwa kuiunga mkono serikali kwa jambo hili jema la kuleta vifaa ambavyo ni vya kisasa zaidi vitakavyoweza kupima mgonjwa na kubaini kama amepata maambukizi ya UVIKO – 19. Hapa Kahama kuna mwingiliano mkubwa wa watu hivyo zitasaidia kupima watu wengi”,amesema Mjema.


Mjema ameutaka uongozi wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama kutumia mashine hizo kwa matumizi stahiki ili viweze kuwasaidia wananchi.


“COVID – 19 bado ipo. Mmepata vifaa hivi, watangazieni wananchi kuhusu uwepo wa mashine hizi waje wapime kwani mashine hizi zinatoa majibu ndani ya saa moja tu. Zitasaidia kuwapunguzia wananchi umbali wa kufuata huduma ya vipimo vya UVIKO – 19 katika Viwanja vya ndege au Jijini Dar es salaam”,amesema Mjema.


Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Daniel Mzee ameishukuru Kampuni ya Barrick kwa kuwapatia mitambo hiyo ya kupimia UVIKO – 19 kwani Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa ambayo ilikuwa imeathiriwa na COVID – 19 katika wimbi la tatu hivyo kuahidi kutunza mashine hizo na kuhakikisha zinatumika kama inavyopaswa.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages