Breaking

Wednesday 23 March 2022

MSIMAMO WA TANZANIA JUU YA MGOGORO WA URUSI NA UKRAINE




Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu sababu ya kupiga kura ya kutofungamana na upande wowote katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine huku ikisisitiza pande zote mbili kutafuta suluhu katika meza ya mazungumzo.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ametoa ufafanuzi huo wakati akifanya mahojiano na mojawapo ya vyombo vya Habari kutoka China na kuongeza kuwa Sera ya Tanzania kuhusu namna ya kutatua changamoto za migogoro inapojitokeza ni kwa kutumia njia za kidiplomasia.

Balozi Mulamula amesema kuwa Sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijabadilika tangu uhuru na kuwa inaamini hakuna mgogoro ambao hauwezi kutatulika hasa panapokuwepo na utashi na nia njema ya kumaliza mgogoro.

Ameongeza kuwa  njia ya kidiplomasia ndio chaguo sahihi kwa Tanzania kuhusu namna bora ya kumaliza mgogoro kati ya Urusi na Ukraine.

“Sisi msimamo wetu na Sera yetu na msingi wetu wa Sera yetu ya Mambo ya Nje ni kutofungamana na pande zozote, hivyo kutokupiga kura ni kuonesha msimamo wa Tanzania,” amesema Balozi Mulamula.


Alipoulizwa juu ya Tanzania kuathirika na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine, Balozi Mulamula amesema madhara yanayotokana na vita hiyo yanajionesha dhahiri huku akitaja baadhi ya madhara hayo kwa baadhi ya wanafunzi wa kitanzania waliokuwa wanasoma nchini Urusi kukatisha masomo yao na kurejea nchini wakisubiria vita kumalizika pamoja na ongezeko la bei ya petroli na gesi duniani.

Kutokana na vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urusi Tanzania ililazimika kuwaondoa raia wake nchini Ukraine hususan wanafunzi takribani 300 waliokuwa wakisomea masuala ya udaktari nchini humo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages