Breaking

Wednesday 23 March 2022

WAZIRI GWAJIMA ATAKA KASI UANZISHWAJI WA MADAWATI YA JINSIA VYUO VYA ELIMU YA JUU

 


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dorothy Gwajima akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo, kilichofanyika jijini Dodoma leo tarehe 23/03/2022.
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum amabye ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula akiendesha kikao cha Bazara la Wafanyakazi la Wizara, kilichofanyika jijini Dodoma leo tarehe 23/03/2022.
Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Christopher Mushi akieleza jambo wakati wa kikao cha Baraza hilo leo tarehe 23/03/2022.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wakifuatilia matukio katika kikao cha Baraza hilo kilichofanyika leo tarehe 23/03/2022.


Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi TUGHE, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Ikusubisya Kasebele akiwasilisha mada kwa niaba ya watumishi wa Wizara hiyo katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika jijini Dodoma leo tarehe 23/03/2022. 

***************

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametaka kuongezeka kasi katika uanzishwaji wa madawati ya jinsia kwenye Vyuo vya Elimu ya Juu na kati kwani kumekuwa na kasi ndogo kuliko ilivyoelekezwa na Serikali.

Dkt  Gwajima amebainisha hilo leo Jumatano Machi 23, 2022 wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo kilichofanyika jijini Dodoma.

Waziri Gwajima amefafanua kwamba, Wizara iliandaa mwongozo na kuratibu uanzishwaji wa madawati haya kwa lengo la kuweka mfumo wa kushughulikia masuala ya unyanyasaji wa kingono na vitendo vya ukatili katika vyuo vya elimu ya juu na kati na kuimarisha ulinzi wa wanawake na watoto dhidi ya vitendo hivyo.

"Katika vyuo hivi nimefuatilia takwimu, kasi ya uanzishwaji wa madawati haya ni ndogo sana, hivi vyuo vilitakiwa vione umuhimu wa uwepo wa madawati haya, nadhani kuwe na mawasiliano kati ya Baraza hili na mabaraza ya vyuo kuona sera ya usawa wa kijinsia katika vyuo inavyotekelezwa" amesisitiza Mhe. Dkt. Gwajima.

Waziri Gwajima ameoneshwa kusikitishwa pia na baadhi ya wafanyakazi wa vyuo kuwa vikwazo vya uanzishwaji wa madawati hayo kwa wao wenyewe kufanya unyanyasaji wa kijinsia.

Ameongeza pia Serikali itahakikisha mwongozo huo unafika hadi katika shule za Msingi na Sekondari ili kusaidia mapambano ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Aidha, Waziri Dkt. Gwajima amesema, Dunia yote kwa sasa inaelekea kwenye kuimarisha usawa wa kijinsia hasa kwenye masuala ya kiuchumi hivyo ametoa wito watanzania kujipanga kupata fursa hizo kupitia Kamati iliyoundwa kuratibu utekelezaji wa ahadi za nchi katika jukwaa la usawa wa kijinsia.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara  Dkt. Zainab Chaula, amemuhakikishia Waziri kuwa Wizara itaendelea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ili kutokomeza vitendo vya ukatili kwani ndiyo msingi katika kuimarisha usawa wa kijinsia.

Dkt. Chaula amesema pamoja na changamoto zilizopo, Wizara imejipanga kushughulikia Ustawi na Maendeleo ya jamii kwa makundi yote kwani ndiyo chachu katika maendeleo ya Taifa.

"Suala la ukatili wa kijinsia tumelishikia bango japo bado halijaongelewa vya kutosha, tutaendelea kwa kushirikiana na wadau. Vilevile kuhakikisha tunatatua changamoto ya uhaba wa watumishi, ukosefu wa ajira na uchakavu wa majengo hasa ya makazi ya wazee" amesema Dkt. Chaula.

Dkt. Chaula ametumia nafasi hiyo pia kumpongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua umuhimu wa usawa wa kijinsia na kuchagua kuwa kinara katika eneo hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi TUGHE katika Wizara hiyo Ikusubisya Kasebele ameshukuru uongozi wa Baraza hilo kwa kufuata sheria na kukaa kikao mara mbili kwa mwaka na kuhusisha wajumbe kutoka maeneo yote yanayosimamiwa na Wizara hiyo.

Kasebele ameongeza kuwa wajumbe wote wana haki ya kuchangia mawazo yao ikiwemo kupitia bajeti iliyoandaliwa kwa maslahi ya Taifa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages