Breaking

Saturday 12 March 2022

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO KUKABILIANA NA UJANGILI BARANI AFRIKA


Na Mwandishi Wetu - Zambia


Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika.


Hayo yamesemwa leo Jumamosi Machi 12, 2022 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mary Masanja  wakati wa hitimisho la mkutano wa 13 wa Baraza la Uongozi  la Mkataba wa Lusaka(The 13rd Governing Council of the Lusaka Agreement) katika kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika uliofanyika jijini Livingston nchini Zambia.


Amesema mkutano huo utafanyika mwezi Mei mwaka 2024 na unatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 100 na utakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania kwa sababu kuna mashirika mbalimbali ambayo yanayojitokeza kuzisaidia nchi za Afrika ambazo zinapambana na ujangili wa misitu na wanyamapori.


Ameongeza kuwa kama Tanzania itafikia masharti yaliyowekwa, kitajengwa kituo cha kupambana na ujangili wa misitu na wanyamapori jijini Arusha lengo ni kudhibiti ujangili wa misitu na wanyamapori na kuhakikisha biashara haramu ya ujangili wa wanyamapori na misitu inakomeshwa.


“Nchi itafaidika na mkutano huo kwa sababu tumekuwa na changamoto kubwa ya mapambano dhidi ya maharamia wanaodhuru wanyama wetu na hivyo tutakomesha biashara haramu.”  Masanja amefafanua.


Akiongelea kuhusu Mkataba wa Lusaka, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Zambia, Hassan Simba Yahya amesema mkataba huo unajihusisha na kuzuia uuzaji, usafirishaji wa wanyamapori pamoja na mimea hivyo utasaidia katika kupambana na ujangili na uhamishaji wa wanyama na mimea ambayo iko katika hatari za kutoweka.


Amesema Tanzania imeshiriki katika mkutano wa 13 wa Baraza la Uongozi  la Mkataba wa Lusaka katika kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika ambao maamuzi yake yatainufaisha Tanzania kama nchi mwanachama.


Mkutano huo umehudhuriwa na Mawaziri Wanachama kutoka nchi za Congo, Lesotho, Liberia, Tanzania, Uganda na Zambia. Nchi zingine zilishiriki kama Waangalizi (Observers) ni Niger, Senegal, Angola, Malawi, Mozambique, Togo, Ivory Coast, Benin, Ghana, Guinea , Burkina Faso na Nigeria.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages