Breaking

Sunday 12 May 2024

MWENGE WA UHURU WAKOSHWA UIMARISHAJI HUDUMA WAZO

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndugu Godfrey Mnzava ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kuboresha huduma ya majisafi katika Wilaya ya Kinondoni kupitia Mradi wa Ujenzi wa mfumo wa usambazaji kutoka Makongo hadi Mji wa Bagamoyo uliotekelezwa mwaka 2022 na kuhudumia wakazi takribani 450,000.

Ndugu Mnzava amesema hayo wakati wa Mwenge wa uhuru kukagua miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Kinondoni ambapo walitembelea kituo cha kusukuma maji Wazo ambao ni sehemu ya mradi wa maji Makongo hadi Bagamoyo na pia kupokea taarifa ya uendelevu wa mradi.

"Malengo ya Serikali ya awamu ya sita ni kumpatia kila Mwananchi maji safi na salama lakini kuyapata maji hayo kwa ukaribu zaidi bila kutumia umbali mrefu na kupitia mradi huu DAWASA mmetimiza malengo hayo”. alifafanua

Ameongeza kuwa ni wajibu wa watendaji sekta ya maji kuhakikisha wananchi wanapata maji na sio vinginevyo, lakini zaidi amesisitiza kuridhika na uendelevu wa mradi kuanzia hatua za utekelezaji hadi kukamilika na kuwataka DAWASA kuendelea kuutunza mradi huo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule ameipongeza DAWASA kwa kufanikisha utekelezaji wa mradi huu mkubwa wa maji ambao unaenda kupunguza adha ya changamoto ya huduma ya maji kwa wananchi wa Wilaya ya Kinondoni.

"Niwapongeze DAWASA kwa kutekeleza mradi huu ambao ni dhamira kuu ya Serikali yetu katika kuhakikisha tunamtua mama ndoo kichwani, mradi huu ni utatuzi wa changamoto za upatikanaji maji Wilaya ya Kinondoni," ameeleza Mhe. Mtambule.

Akisoma taarifa ya mradi Kwa kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa, Mhandisi Gloria Swai amesema kuwa Mradi umesaidia kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji katika Kata za Wazo na Goba na katika mitaa 11 ya Mivumoni, Kilimahewa, Kisanga, Madale, Tegeta A pamoja na Kinzudi.

Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 umebeba kaulimbiu isemayo "Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu."





Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages