
Na Samir Salum-lango la habari Blog
Jeshi Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Mwanamke mmoja kwa tuhuma za mauaji ya Mtoto wa Mdogo wake aliyekuwa na umri wa miaka miwili (2) na miezi minne.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ACP Muliro Jumanne Muliro amesema kuwa mnamo April 05, 2022 Mtuhumiwa huyo ambaye ni LATIFA BAKARI Mwenye Umri wa Miaka 33 mkazi wa Mabibo aliachiwa mtoto huyo na mdogo wake kwa lengo la malezi ambapo alitekeleza mauaji hayo baada ya kumpiga kupita kiasi.
Kamanda Muliro amebainisha kuwa baada ya kubaini kuwa mtoto huyo amefariki kwa kipigo mnamo April 06, 2022 aliuchukua mwili wa mtoto (marehemu), akaukunja na kuuweka kwenye ndoo ya plastiki kisha kuudumbukiza kwenye kiroba na kwenda kuutupa eneo la River Side UBUNGO.
Ameongeza kuwa Baada ya majirani kutomuona mtoto huyo kama ambavyo si kawaida walitoa taarifa Polisi, ambapo Polisi ilimuhoji kwa kina mtuhumiwa huyo na akakiri kufanya mauaji hayo na kwenda kuwaonesha Polisi mwili wa mtoto huyo ulipokuwa.
Mwili huo umepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi na mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani haraka iwezekanavyo baada ya mifumo ya kisheria kukamilika.