Breaking

Friday 22 April 2022

MBUNGE LUSINDE AMVAA ZITTO, AMTAKA AIOMBE MSAMAHA FAMILIA YA MAGUFULI






Mbunge wa Jimbo Mvumi Livingstone Lusinde amemtaka kiongozi wa Chama Cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe awaombe radhi Watanzania pamoja na familia ya hayati Dkt. John Magufuli Kwa kitendo Cha kumsema vibaya aliyekuwa Rais wa awamu ya tano hayati Dkt. John Magufuli.

Lusinde ameyasema hayo Leo Ijumaa April 22, 2022 Bungeni jijini Dodoma, ambapo ameeleza siyo jambo jema kumsema marehemu ikizingatiwa Zitto ni muislam anaelewa makosa ya kumsema marehemu.

Zitto alisema wanaompenda Magufuli waende kuzikwa naye, kauli ambayo Lusinde ameipinga vikali akisema kuwa Zitto anatakiwa kuomba radhi kwani hata chama chake kilimpoteza Mwenyekiti, Maalim Seif Sharif Hamad lakini wao hawamuombei mabaya.

"Zitto anatutaka tunaompenda Magufuli tukazikwe naye, Waislamu mmefunga, dini inakataza kuwasema vibaya marehemu na yeye ni Muislamu anajua, ametukosea sana, atuombe radhi Watanzania, Zitto amemkosea sana Mama Magufuli na ameikosea familia"- Amesema Mbunge Lusinde
Lusinde amesema mtu mmoja alisema kwa vitendo kuwa hawezi kufanya kazi na Magufuli naye alikuwa ni Nyalandu (Lazaro Nyalandu aliyewahi kuwa Mbunge wa Singida Kaskazini na Waziri wa Maliasili na Utalii).

“Lakini wote tuliobaki hapa ni watu wa Magufuli, na tulifanya naye kazi na tulikuwa tunamsifu na hivyo ndivyo tunatakiwa kumsifu na mheshimiwa Samia (Rais Samia Suluhu Hassan). Ndio kazi tunayoifanya hapa hatufanyi unafiki.

Nataka nikwambie hawa watu wanaomsema vibaya Magufuli na kumsifu Rais Samia ni wanafiki wakubwa. Samia akiondoka watamsema vibaya hivyo hivyo, ni bora mimi Lusinde niko wazi. Na siwezi kuacha haiwezekani.”amesema.

Amesema kwamba ili nchi iendelee utawala bora watu wote ni lazima kushirikiana nao na kwamba hao waliofariki dunia ni watu wazito.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages