Breaking

Sunday 17 April 2022

MEGAWATI 200 ZA JOTOARDHI KUZALISHWA KABLA YA MWAKA 2025

 


Na Selemani Msuya, Mbeya

SERIKALI imesema katika kuhakikisha adha ya kukatika umeme inaisha inatarajia kuzalisha megawati 200 zinazotokana na chanzo Cha Jotoardhi kabla ya mwaka 2025.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, wakati wa ziara yake ya kukagua vyanzo vya nishati ya Jotoardhi vya Kiejo-Mbaka na Ngozi mkoani Mbeya.

Amesema Tanzania kuna jumla ya maeneo 52 yanayoweza kutoa nishati ya Jotoardhi ambayo tayari yameshatambuliwa, hivyo watayatumia kutimiza lengo Hilo la kuzalisha Megawati 200 ifikapo 2025.

Ameeleza kuwa, kwa ujumla, Serikali ina mpango wa kuongeza megawati 1,100 zinazotokana na Nishati Jadidifu kabla ya mwaka 2025 na hizo megawati zitatokana na vyanzo mbalimbali kama vile Jotoardhi, Jua na Upepo.

Ameongeza kuwa, Wizara ya Nishati inaweka nguvu kubwa katika kuendeleza vyanzo vya nishati ya Jotoardhi kwa sababu vyanzo hivyo haviishi na hivyo ukaguzi alioufanya katika maeneo hayo ya Jaothemo utasaidia Serikali kuona hatua stahiki za kuchukua ili kuendeleza vyanzo hivyo.

“Kipindi cha ukame maji yanaweza kupungua, lakini Jotoardhi katika kipindi cha ukame au mvua, mvuke unaotoka chini ya ardhi uko palepale,"  amesema Katibu Mkuu Mramba.

Amesema kuwa, nchi ya Kenya ina zaidi ya megawati 1,100 zinazotokana na Jotoardhi na Tanzania kutokana na eneo lake kubwa kupitiwa na Bonde la Ufa kuna uwezekano wa kupata umeme mwingi zaidi unaotokana na nishati hiyo.

“Mfano hapa mkoani Mbeya katika eneo hili la Rungwe kumeonekana kuna uwezekano mkubwa wa kutoa nishati ya Jotoardhi kwa sababu tawi moja la Bonde la Ufa limeingia katika eneo hili na Tawi jingine limeelekea upande wa Malawi," ameeleza Mhandisi Mramba

Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba amesema kuwa, eneo la Kiejo-Mbaka linaweza kuzalisha megawati 60 zinazotokana na Jotoardhi.

Amesema kuwa, Serikali imetoa takribani Sh.bilioni 20 kwa ajili ya uendelezaji wa eneo hilo na sasa wamenunua mtambo wa kuchoronga eneo hilo, na kwamba, wataalam wa TGDC na wahisani wameshirikiana katika kufanya tafiti zote zinazotakiwa.

Ameongeza kuwa katika eneo la Ngozi, inategemewa kuwa litazalisha megawati 70 zinazotokana na Jotoardhi na kwamba TGDC imejipanga vizuri katika kuhakikisha kuwa Tanzania inapata umeme kutoka kwenye nishati hiyo Jadidifu.

Mwisho


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages