
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameliagiza jeshi la polisi wilayani Handeni kuwakamata na kuwaweka ndani watumishi wawili wa wizara hiyo na mkandarasi anayejenga bwawa la Kwenkambala kwa kushindwa kumpa taarifa sahihi kuhusu ujenzi wa bwawa hilo.
Waziri Aweso ametoa agizo hilo leo Jumanne April 12 kwenye ziara yake ya kukagua ujenzi wa bwawa la maji la Kwenkambala na miradi ya maji katika kijiji na Msomera,ambapo wasimamizi wa mradi wa Kwenkambala kutoka Ruwasa na Mkandarsi walishindwa kutoa taarifa alizotaka waziri na kuagiza wakamatwe.
Waliokamatwa na jeshi la polisi ni mtaalamu wa bwawa kutoka Ruwasa Hamisi Matunguru,mkandarasi Robert Lupinda na Mhandisi Amos Mtweve mthibiti ubora kutoka makao makuu ya Ruwasa.
Waziri amesema kuwa fedha zilipelekwa watu wapate huduma ya maji ila kwa makusudi kuna waliohujumu fedha za mradi na kushindwa kuendelea mpaka sasa.
"Kwa wataalamu wetu ambao kwa makusudi wanaendeleza hizi hujuma sitasita kuwachukulia hatua,hata awe mkubwa vipi lazima atachukuliwa hatua,niombe radhi kwa wananchi na viongozi wa Handeni kwa hili lililotokea",
Mkandarasi Robert Lupinda kwa upande wake amesema amesimama kuendelea na ujenzi wa bwawa hilo baada ya kusimamishwa.
Kwa upande wa viongozi kutoka Ruwasa alioagiza wakamatwe Waziri Aweso amesema kesho Jumatano atakaa kikao na wataalam wengine Dodoma ili kujua shida iko wapi na atachukua hatua.
Source: Mwananchi