Breaking

Saturday 7 May 2022

AFRICAN COUSINS (TASUBA) WASHINDI UNITALENT 2022, WAONDOKA NA MILIONI 10, SERIKALI KUWAPIGA MSASA BURE WASHIRIKI WOTE




Kikundi cha African Cousins kinachoundwa na vijana sita kutoka TaSUBa kimeibuka Kinara katika mashindano ya vipaji kwa wanavyuo ya Uni Tarent.


Kikundi hicho kimeibuka kinara dhini ya washindani 12 katika kilele cha shindano hilo la wasanii kutoka vyuo mbalimbali nchini la Uni Talent Show liliofanyika usiku wa kuamkia leo Mei 07, 2022 katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.


Akizungumza katika mashindano haya Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali kupitia Wizara imewatunikia zawadi ya kupewa mafunzo maalum ya fani za washiriki wote wa Uni Talent Show wa 2022 katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ili wapigwe msasa kuongeza ubunifu katika sanaa zao.




Waziri Mchengerwa amewapongeza waandaaji wa shindano hilo na kufafanua kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ina dhamira ya dhati ya kuinua na kukuza taaluma na kazi za wasanii ili waweze kufaidika na kazi zao.


“Jukumu la Serikali katika sanaa ni kukuza vipaji vya watu wake, hivyo napenda kuwaahidi hapa kwamba wote walioshiriki tunakwenda kuwapiga msasa na kuwanoa kule TaSUBA ili wafike mbali” amesisitiza Waziri Mchengerwa.



Ameagiza Wizara yake kuhakikisha Taasisi ya Maroon Entertainment iliyoandaa shindano hilo kushirikishwa katika program maalum ya Serikali ya kuibua vipaji uliopewa jina la Mtaa kwa mtaa unaotarajiwa kuanza kutekelezwa punde mara baada ya vikao vya Bunge la Bajeti.


Akizungungumzia kuhusu falsasa ya ya kipaji chako ndicho kiwanda chako amesema amefurahishwa na falsafa inayosisitiza vijana kufanya kazi kwa kujituma na kuongeza weledi ili kufikia mafanikio huku akiwataka kuacha uzembe.



Katika hatua nyingine, Mhe. Mchengerwa alinunua picha ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa shilingi laki tano iliyochorwa mubashara jukwaani kwa kutumia takribani dakika tatu tu kwenye shindano hilo na msanii Amour Abdallah kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro.


Waziri Mchengerwa amekikabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 10 za kitanzania kikundi cha African Cousins kinachoundwa na vijana sita ambao ni Rahimu Rajabu, Leonard Mathias, Miriam Fredirock, Allain Moses, Baraka Bukuk, na Joshuan Paul, wote wanafunzi wa TaSUBa.


Shindano hilo lilipambwa na wasani mbalimbali wa muziki wakiongozwa na Barnaba na kuwafanya watazamaji kushangilia muda wote wakati wasanii washiriki wakipanda jukwaani kuonyesha kazi zao ambazo zilikuwa na ubora na ushindani mkubwa.



Shindano hili ni jukwaa mahususi kwa ajili ya kuibua vipaji vya wanafunzi wa vyuo na kwa sasa ni la tatu tangu kuanza kuandaliwa ambapo limevuta hisia kali kwa watu mbalimbali duniani kuendelea kulifuatilia.


Kwa msimu huu wa tatu; vyuo 100 vilifikiwa na kuwezesha kupata washabiki 150,000 katika mitandao ya kijamii; pia ilipata kutazamwa mara 200,000 kupitia mitandao ya kijamii hususan youtube.



Mbali na zawadi ya Serikali ya kuwanoa washiriki wote, zawadi nyingine zilizotolewa na waandaaji ni pamoja na shilingi milioni 10 kwa mshindi/kikundi wa kwanza na nafasi ya kwenda kujiendeleza kimasomo nchini Uholanzi kwa kozi fupi, Shilingi millioni 3 kwa mshindi wa 2 na milioni 1 kwa mshindi wa 3.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages