Breaking

Friday 27 May 2022

BABA NA MTOTO WAHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA KWA KOSA LA MAUAJI - MUSOMA




Mahakamani Kuu Kanda ya Musoma kupitia Mahakama ya Wilaya Tarime Mkoani Mara imewahukumu baba na mtoto wake wa Kijiji cha Genkuru kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya mauaji.

Waliohukumiwa ni Matinde Keranganyi (baba) na Mwita Matinde (mtoto) ambao walishtakiwa kwa kumpiga mawe, kumkata mapanga na kumchoma mkuki Chacha Nyamhaga, wakigombea ardhi.

Hukumu hiyo ilisomwa na Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Frank Moshi.

Awali, Mwanasheria wa Serikali, Yese Temba, alidai kuwa washtakiwa Mei 25, 2019 kwa makusudi wakiwa na silaha za jadi walimvamia Nyamhanga akiwa shambani kwake kumshambulia kwa kumpiga mawe na kuanguka chini na kisha kumchoma mkuki na kumkata mapanga kichwani hali iliyosababisha kifo chake.

Chanzo cha mauaji hayo kimedaiwa kuwa ni mgogoro wa ardhi kati ya marehemu na washtakiwa hao.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Mwanasheria wa Serikali Temba ulileta mashahidi saba vikiwamo vielelezo na PF3, mganga aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu na upande wa utetezi ulileta mashahidi wanne.

Msajili wa Mhakama Kuu, Moshi alisema Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka bila kuwapo shaka lolote.


Source: Nipashe
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages