Breaking

Friday 27 May 2022

TANZANIA YAANZA MAANDALIZI YA KURATIBU MASHINDANO YA AFCON


Na John Mapelele

Serikali ya Tanzania na Qatar zimefanya mazungumzo kuratibu mashindano makubwa ya Afrika ya Soka hususan Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON ifikapo mwaka 2027.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa kwa upande wa Serikali ya Tanzania na Balozi wa Qatar nchini, Hussain Ahmad Al-Homaid leo Mei 27, 2022 Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.

Waziri Mchengerwa amesema kuwa lengo ni kuimarisha mahusiano kwenye sekta za utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo  yanalenga kusaidia Tanzania  kufanya mapinduzi makubwa  kwenye sekta ya michezo nchini.

Amesema kuwa tayari Serikali imeshaomba  miundombinu ya soka inakayotumika kwenye  mashindano ya kombe la Dunia yanayotarajiwa  kufanyika nchini Qatar ambapo Mhe, Balozi Al-Homaid amesema  Serikali yake itazingatia ombi hilo kwa kuipa kipaumbele nchi ya Tanzania.

“Maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na dhamira  ya Serikali kuona kuwa Tanzania inakwenda  kuratibu AFCON 2027” amefafanua Mhe Mchengerwa.

Ameongeza kuwa Serikali imejipanga  kuboresha na kujenga  miundombinu ya kisasa  ikiwa ni pamoja na viwanja vitatu ambayo vitasaidia Tanzania  kufuzu  vigezo  vya kupata nafasi ya kuratibu  mashindano haya.

Aidha, katika kuimarisha ushirikiano baina  ya nchi yetu na Qatar, amesema Wizara inakwenda kuandaa tamasha kubwa la wasaanii  ikiwa ni pamoja na wasanii wa  uchoraji na uchongaji  ambapo  amefafanua kuwa Tanzania ina hazina kubwa  ya wasanii ambao wamekuwa  wakitengeneza  kazi nzuri zinazouzwa kwa  thamani kubwa duniani.

Baada ya mazungumzo hayo ambayo Waziri Mchengerwa akiambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi na Naibu Katibu Mkuu Saidi Yakubu na Mkurugenzi wa Michezo nchini Yusufu Singo alipata fursa ya kukagua miundombinu ya Uwanja wa Benjamini Mkapa na  Mashindano ya Afrika ya Riadha ambayo yamekuwa yakiendelea uwanjani  hapo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages