Breaking

Tuesday 31 May 2022

WATU 100 WAFARIKI, 40 WAJERUHIWA MAPIGANO YA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI



Mapigano kati ya wachimba madini wadogo, yaliyodumu ndani ya juma moja kaskazini mwa Chad yamesababisha takriban watu 100 kupoteza maisha na 40 kujeruhiwa, na kupelekea machimbo hayo kufungwa kwa muda usiojulikana


Mapigano hayo yalitokea Mei 23 na 24 katika wilaya ya Kouri Bougoudi, karibu na mpaka na Libya eneo ambalo lina migodi mingi ya dhahabu


Akizungumza na waandishi wa habari Mei 30, 2022 Waziri wa ulinzi wa Chad, Daoud Brahim amesema kuwa kwa mujibu wa ujumbe wa serikali zaidi ya watu 100 waliuawa na wengine 40 kujeruhiwa katika mapigano hayo.


Waziri Brahim amesema mapigano yalizuka usiku katika maeneo ya uchimbaji madini, lakini hakubaini chanzo cha ghasia hizo.


Waziri wa mawasiliano wa Chad alisema wiki iliyopita kwamba mapigano hayo yalikuwa kati ya Waarabu waliovuka mpaka kutoka Libya na jamii ya Tama wanaotoka mashariki mwa Chad.


Mamlaka ya Chad imesitisha shughuli zisizo rasmi za uchimbaji madini huko Kouri Bougoudi na kuwahamisha watu kutoka eneo hilo.


Aidha, Mahamat Nour Ibedou, mkuu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Chad, amelishutumu jeshi la nchi hiyo kwa kudai wanajeshi waliotumwa kuingilia kutuliza ghasia waliwafyatulia raia risasi


Chad inashiriki katika mapambano dhidi ya ugaidi na makundi ya waasi wanaotishia kupindua serikali ya mpito inayoongozwa na mtoto wa marehemu rais Idriss Deby. Hata hivyo, hakukuwa na dalili kwamba makundi ya kigaidi au ya wahalifu yalihusika katika ghasia za uchimbaji madini.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages