Breaking

Thursday 23 June 2022

BRELA, FCC NA SIDO ZASAINI MAKUBALIANO YA KUSHIRIKIANA KUBORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI

Na Lango La Habari 


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imesaini makubaliano ya ushirikiano na Tume ya  ushindani  (FCC), wakati huo huo  FCC ikisaini na  Shirika  la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), yenye lengo la kuboresha mazingira  uwekezaji nchini.


Akizungumza mara baada ya utiaji saini makubaliano ya ushirikiano huo Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amesema BRELA  ipo tayari kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa mbalimbali pale zinapohitajika.


Bw. Nyaisa amesema kuwa ushirikiano wa taasisi hizo za Serikali ambazo zinawezesha biashara  utatoa fursa kwa wawekezaji kupata masoko ya uhakika huku bidhaa zao zikiwa zinatambulika na Mamlaka husika. 


"Ndugu wanahabari tunaomba muufahamishe Umma wa Watanzania na wawekezaji  kuwa utiaji saini huu  unalenga kufungua milango zaidi ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuondoa migongano ya hapa na pale ambayo inaweza kuchelewesha michakato ya urasimishaji wa biashara, hivyo  tunafanya haya kuhakikisha  wawekezaji wanakamilisha michakato ya ufanyaji Biashara kwa wakati," amefafanua Bw. Nyaisa.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu  wa FCC, Bw. William Erio amesema yanapotokea malalamiko ya mtu kutumia alama  ya biashara ya mwingine FCC huomba taarifa kutoka BRELA kwani ndiyo yenye dhamana ya kusajili majina ya biashara, kampuni na alama za biashara.


Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Profesa Sylvester Mpanduji amesema SIDO kama mlezi wa viwanda vidogo itahakikisha inatoa ushauri na kuhimiza wadau wanaopata mafunzo kurasimisha biashara zao BRELA, ili  kukidhi vigezo katika soko la ndani na nje ya nchi.


Utiaji saini makubaliano hayo yamefanyika tarehe 23 Juni, 2022 katika ofisi za FCC, Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Waziri mwenye dhamana ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, yanayozitaka Taasisi chini ya Wizara hiyo, kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuvutia wawekezaji na kufanya Tanzania kuendelea kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI 

Afisa mtendaji mkuu wa wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw Godfrey Nyaisa kulia akitia Saini makubaliano ya ushirikiano na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani   (FCC) Ndg.William Erio ili kurahisisha mazingira ya wawekezaji nchini.





Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages