Breaking

Monday 13 June 2022

BRELA YAJA NA MWAROBAINI WA MIGOGORO KWENYE MAKAMPUNI

Na Lango La Habari, Dar es Salaam 


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) inakutana na wadau wenye migogoro katika kampuni mbalimbali ili kuwezesha kampuni hizo kufanya kazi kama ilivyokusudiwa katika uanzishwaji wake.


Akizingumza katika siku ya kwanza ya wiki maalum ya "Suluhisha na BRELA" inayofanyika katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, uliopo Mtaa wa Shaaban Robert, Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Makampuni na Majina ya Biashara kutoka BRELA, Bw.  Meinrad Rweyemamu amesema, kampuni zinaweza kuendeshwa bila  migogoro endapo  uendeshwaji wake utazingatia Sheria.


Rweyemamu amewataka wamiliki wote wa kampuni ambao wanakumbana na changamoto katika uendeshaji wa kampuni zao, kufika na kupatiwa huduma, kwani Msajili ametoa muda wa wiki moja ambapo migogoro katika kampuni itapatiwa  ufumbuzi kwa kushauriana na wataalamu kutoka BRELA.


“BRELA ni mlango wa kufungua biashara hapa nchini, lakini pia ni kitovu cha uwekezaji na taarifa zote za wamiliki zipo kwetu, lakini mabadiliko yoyote yanapofanywa katika kampuni  yanapaswa kuridhiwa na wahusika, vinginevyo huwa ni chanzo kimojawapo cha migogoro katika kampuni, " amefafanua Bw. Rweyemamu.  

Ameongeza kuwa wakati mwingine mwanahisa  wa Kampuni, hisa zake zinaweza kutaifishwa au kutolewa kwenye umiliki wa kampuni  bila ya kufuata utaratibu, hivyo  katika wiki hii ya suluhisha na BRELA wote wenye changamoto za namna hiyo  wafike na kupatiwa  ufumbuzi.


Aidha amewataka wale wote ambao wazazi wao  wamefariki na kudhulumiwa hisa zao au haki zao za msingi, wafike katika "Suluhisha na BRELA" yote yatafanyiwa kazi kwa mujibu wa Sheria.


"Suluhisha na BRELA" ni kampeni maalum ya wiki moja inayofanyika tarehe 13-19 Juni, 2022 kwa lengo la kutatua migogoro  kwenye kampuni ili ziwe huru kijiendesha kulingana na lengo la uanzishwaji wake.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages