Breaking

Thursday 16 June 2022

MILIONI 160 KUKAMILISHA UJENZI WA HOSTEL YA WANAFUNZI WA KIKE SHULE YA SEKONDARI BWANJAI KAGERA

Na Lydia Lugakila, Lango La Habari, Kagera


Jumla ya shilingi milioni 160 zinatarajia kutumika katika kukamilisha ujenzi wa hosteli ya wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Bwanjai iliyopo Kata ya Bwanjai  wilayani Misenyi Mkoani Kagera.


Akizungumza na Mwandishi wa habari hii, Mkuu wa shule ya sekondari Bwanjai, Donatus Leonard amesema kuwa kujengwa kwa hosteli hiyo kumetokana na nguvu za umoja wa wakazi wa kata ya Bwanjai lengo ikiwa ni kuepusha changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wanafunzi wa kike wanaosoma shuleni hapo. 


Leonard ametaja changamoto hizo kuwa ni  wanafunzi hao kutembea umbali mrefu wa kilometa 15 kuifuata shule hiyo hali inayohatarisha usalama wao.


"Wakati mwingine wanafunzi hawa husinzia darasani wakati wa masomo kutokana na kuchoka baada ya kutembea umbali mrefu" amesema Mwalimu Mkuu


Amesema kuwa hadi sasa jumla ya shilingi milioni 52 zimeishatumika huku milioni 102 zikihitajika ambapo tayari Serikali Wilayani Misenyi imeahidi kuchangia kiasi cha shilingi milioni 20.


Aidha, ameongeza kuwa  ujenzi huo umefikia hatua ya renta ambapo hosteli hiyo itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 80.


Kwa upande wake katibu wa umoja huo Prasidius France amewashukuru wananchi kwa kujitoa kusaidia ujenzi huo huku akiwaomba wadau mbalimbali kujitokeza ili  kuwezesha hostel hiyo kukamilika.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages