Breaking

Thursday 23 June 2022

MMUYA APONGEZA HATUA UJENZI OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA DODOMA

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bwa. Kaspar Mmuya (katikati) akikagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi hizo Kilimani  Jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu  Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bwa. Kaspar Mmuya (wa tatu kushoto) akiangalia mchoro wa ramani ya jengo la ofisi za Msajili wa vyama vya siasa zinazojengwa  eneo la Kilimani Jijini Dodoma .
Naibu Katibu Mkuu  Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bwa. Kaspar Mmuya (wa kwanza mbele) akiangalia  mpango kazi wa ujenzi wa  jengo la ofisi za Msajili wa vyama vya siasa Kilimani Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa nchini Bwa. Magohu Zonzo akifafanua jambo wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) alipotembelea na kukagua ujenzi huo.

**************

Na mwandishi wetu,Dodoma

Naibu Katibu Mkuu  Ofisi ya Waziri Mkuu  anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Bwa. Kaspar Mmuya amepongeza maendeleo ya ujenzi wa ofisi  za  msajili wa vyama vya siasa  nchini zinazojengwa eneo la Kilimani  Jijini Dodoma zitakazogharimu  zaidi ya shilingi bilioni 20.


Naibu Katibu Mkuu huyo aliyasema hayo alipofanya ziara ya kutembelea  na  kukagua ujenzi huo unaofanywa na kampuni kutoka China ya Group Six International Limited ukisimamiwa na  mshauri kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi.


Alisema ujenzi  unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 12 akisisitiza kuongezwa kwa rasilimali watu, muda wa kazi pamoja na vifaa ili kufanya kazi ndani ya muda uliopangwa.


“Niwapongeze kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya Ofisi ya Msajili wa vyama vya sisisa  kwa usmamizi mkubwa mnaoufanya lakini endeleeni kuongeza umahiri na kuwasaidia wenzetu wa Group Six  International wafanye kwa matokeo zaidi,” alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.


 Pia aliamuagiza mshauri wa ujenzi kufika mara kwa mara katika eneo la mradi  na kufanya kazi kwa kushirikiana na watendaji wengine  kufahamu hali ya ujenzi na kutatua changamoto pindi zinapojitokeza kuhakikisha jengo linajengwa katika hali ya uimara, ubora na usalama.


“Nimshauri mtaalamu wetu awe anatembelea mara kwa mara jengo hili kujionea maendeleo ya kazi kama kuna shida yoyote inatatuliwa  kwa wakati na kufanya marekebisho yanayaotakiwa,”alisisitiza .


Aidha aliwahimiza kuongeza ubunifu wa utendaji kazi kwa kugawa maeneo na muda wa kukamilika kwa kazi kwani itasaidia kuhamasisha kazi kufanyika kwa mwamko na ubora zaidi kama njia ya kuendana na muda wa mkataba unavyotaka.


“Waongeze mtindo wa kufanya kazi kwa kupewa kipande cha kazi kwa muda inasaidia utendaji wa kazi na waangalie ubora usiathiriwe kwa sababu mtu anapopewa eneo lake na muda wa kikomo inamfanya ajitume kwa kasi kubwa,” alieleza Bwa. Mmuya.


MWISHO

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages