Breaking

Tuesday 14 June 2022

RC MWANZA AZITAKA HALMASHAURI KUTENGA FEDHA ZA MIRADI YA LISHE KUSAIDIA JAMII






Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel ameziagiza Halmashauri mkoani humo kutenga na kupeleka fedha za miradi ya Lishe kwa wakati ili kutekeleza Afua za Lishe na kuweza kusaidia jamii kuwa na afya bora na kuondoa Udumavu kwa watoto.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Mwanza imeeleza kuwa Mhandisi Robert Gabriel amesema hayo leo Juni 13, 2022 wakati akifungua kikao cha kupitia utekelezaji wa mkataba wa lishe, kupata taarifa ya Kampeni ya Chanjo ya Polio na Maandalizi ya kampeni ya Chanjo ya Uviko 19 kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Aidha, amewataka Maafisa Lishe kutoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi la Afua za Lishe kwenye ofisi za Wakuu wa Wilaya kila wiki zikionesha mafanikio na changamoto kwenye wiki husika ili kwa kushirikiana na Halmashauri waweze kufanikisha kampeni hiyo.

Kuhusu utekelezaji wa kampeni ya Chanjo ya Ugonjwa wa Polio Mhe Mkuu wa Mkoa amewapongeza wadau na viongozi kwa kufanikisha Chanjo hiyo kwa watoto zoezi ambalo yeye mwenyewe ndiye alizindua rasmi wilayani Ukerewe.

Vilevile, Chanjo ya Uviko 19 imeonesha Ukerewe kuongoza kwa idadi ya watu waliochanjwa hadi sasa kwa zaidi ya asilimia 65 na ndipo Mkuu wa Mkoa aliwapongeza na akatoa wito kwa Halmashauri ya Misungwi kuongeza nguvu kwenye zoezi hilo kwani wana asilimia 27 tu.

"Ni kweli kwamba utekelezaji wa Afua za lishe hauendi vizuri kutokana na fedha kutoelekezwa kwenye eneo hilo ila nakuhakikishia Mhe Mkuu wa Mkoa kwenye bajeti mpya ya mwaka wa fedha ujao tutahakikisha shughuli zote za lishe zinakwenda vizuri." Mganga Mkuu wa Mkoa, Dktr Thomas Rutachunzibwa.

Baadae iliwasilishwa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa Hospitali za Halmashauri huku Ilemela wakifikia asilimia 95 hatua ya umaliziaji huku Misungwi wakifikia asilimia 47 pamoja na Kwimba ambao amewataka kuharakisha ujenzi bila kusahau mifumo ya TEHAMA hadi kufikia Juni 30, 2022.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages