Breaking

Monday 4 July 2022

JAMAA AMUOA MAMBA WA MIAKA 7, AMBUSU HADHARANI


Meya wa mji mdogo wa Mexico Victor Hugo Sosa amefunga ndoa na mamba mwenye umri wa miaka saba.

Sherehe hiyo ya mfano ilifanyika San Pedro Huamelula, mji ulioko kusini-magharibi mwa jimbo la Oaxaca kwenye Pwani ya Pasifiki ya Mexico.

Kabla ya tukio hilo, Alhamisi ya wiki iliyopita, mamba huyo alibatizwa na anatambulika kwa jina la Princess, siku iliyofuata Ijumaa ndipo ndoa ikafungwa ambapo bwana hurusi alimbusu mamba huyo mdomoni ingawa mamba alikuwa amefungwa mdomo asije kukinukisha katikati ya sherehe na kujeruhi watu.

Watu walikula, kunywa na kusaza huku muziki ukipigwa na watu kuserebuka.


Mama mtu mzima kwa jina la Elia ambaye alipewa kazi kuhakikisha harusi hiyo inaenda vizuri, amekaririwa akisema aliumiza sana kichwa kujua mamba huyo bibi harusi atavaa nini lakini hatimaye alipata gauni zuri na shela vilishoneshwa kwa ajili ya mamba huyo na kumpendeza vilivyo.


Wanakijiji hawakuishia kula na kucheza muziki tu, bali pia walipata nafasi ya kumbeba na kumshika bibi harusi huyo kwa jina la Princess na kuzunguka nae mitaani kwa furaha.

Pamoja na hayo, harusi hiyo ni ya kimila, mamba anaolewa ambapo watu wa kijiji husika wanaamini kuwa ni muunganiko wa nguvu za kibinadamu na nguvu za kimungu hivyo wanaamini wavuvi maeneo yao watavua samaki wengi, watavuna mazao mengi, kupata chakula kingi, mvua nyingi kunyesha na kila aina ya neema.


Jimbo la Oaxaca lililo kusini mwa Meksiko lina utamaduni mwingi wa kiasili na ni nyumbani kwa zaidi ya makundi kumi na mbili ambayo yanatokana na watu waliokuwa wakiishi katika eneo hilo kabla ya ukoloni wa Uhispania. Vikundi hivi vimehifadhi lugha na mila zao hadi leo.

Kulingana na Taasisi ya Kitaifa ya Takwimu na Jiografia ya Mexico, Oaxaca ina asilimia kubwa zaidi ya watu asilia katika kaunti hiyo kufikia 2020—ikifikia karibu asilimia 70 ya wakazi.


Mamba huchukuliwa kuwa mungu anayewakilisha Mama Duniani, huku ndoa yenyewe ikiaminika kuleta furaha katika mji huo, ambao unategemea zaidi kilimo na uvuvi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages