Breaking

Tuesday 5 July 2022

SOKO LA ASALI LAZINDULIWA TABORA


Na Lucas Raphael,Tabora


SOKO la kwanza la kuuza na kununua asali mbichi iliyochakatwa limezinduliwa katika halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora na kushuhudia ndoo zaidi ya 300 zenye kilo 30 kila moja zilizoletwa na wazalishaji kutoka vijiji mbalimbali wilayani humo zikiuzwa na kununuliwa.

Katika soko hilo kilo zaidi ya 9,000 za asali zenye thamani ya zaidi ya sh mil 36 ziliuzwa na kunuliwa na wadau mbalimbali.

Soko hilo la aina yake limezinduliwa Julai 03, 2022 na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian katika Kijiji cha Lumbe kata ya Ukumbisiganga Wilayani humo ambapo lilihudhuriwa na Wakuu wa Taasisi, wadau wa maendeleo na wanunuzi.

Balozi Batilda ameupongeza uongozi wa wilaya hiyo kuanzia Mkuu wa wilaya, Mkurugenzi, Mwenyekiti wa halmashauri, madiwani na wataalamu wote kwa maono na ubunifu mkubwa wa kuanzishwa soko hilo.

Alisema licha ya asali ya Mkoa huo kupendwa sana na watu wengi ndani na nje ya nchi changamoto kubwa ilikuwa ukosefu wa soko la uhakika hivyo kuanzishwa soko hilo ni mkombozi kwa wananchi wote wanaojishughulisha na ufugaji nyuki.

Aliwataka wazalishaji wa zao hilo kutouza asali yao nje ya soko hilo ili kuepuka kuibiwa na walanguzi, aidha ili kuongeza thamani ya asali hiyo aliwataka kutumia vifungashio vipya na kuweka lebo yenye nembo ya Tabora ili kuitangaza zaidi.

Balozi Batilda alisisitiza kuwa Mkoa huo una uwezo wa kuzalisha asali nyingi zaidi kwa kuwa una maeneo mengi ya misitu ya hifadhi inayofaa kwa shughuli za ufugaji nyuki, hivyo akatoa wito kwa Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi kuhamasisha jamii kuanzisha mashamba ya ufugaji nyuki.

Aidha alimpongeza Mkurugenzi wa Kampuni ya Third Man Co.Ltd Isabella Vonoertzen ambaye ni mdau mkubwa wa kununua asali inayozalishwa katika wilaya hiyo na kuiuza katika nchi za Ujerumani, Italia, Ubeligiji na Uingereza.

Bi.Isabella alisema katika kipindi cha miaka 4 tangu aanze kununua asali ya wakulima wa Wilaya hiyo hadi sasa ameshanunua kilo 270,000 kutoka katika vijiji mbalimbali na ameshalipa zaidi ya sh mil 891.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Mwaga alisema soko hilo ni fursa muhimu sana kwa wakazi wa wilaya hiyo kwa kuwa wataongeza mizinga ili kuvuna asali nyingi zaidi na kujipatia kipato cha uhakika.

‘Soko hili ni muhimu sana kwa kuwa litainua uchumi wa wananchi na kuongeza mapato ya halmashauri na taifa kwa ujumla, halmashauri itaendelea kuwasaidia kwa kuwapa elimu ya ufugaji bora ili kuongeza uzalishaji’, alisema.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Jafael Lufungija alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuteua viongozi wenye maono mazuri ya kusaidia wananchi na kuongeza kuwa maono ya kuanzishwa soko hilo yametokana na dhamira njema ya serikali ya kuwainua wananchi kiuchumi.

Aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na viongozi ili mambo mazuri yote yanayofanyika yawanufaishe, aidha alishauri vikundi vyote kupewa elimu ya ufugaji bora wa nyuki ili kuzalisha asali inayokubalika kimataifa.

Mwisho.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages