Breaking

Friday 29 July 2022

SERIKALI KUANZISHA DAWATI LA JINSIA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANAWAKE SEKTA YA UVUVI

Baadhi ya wanachama wa Mtandao wa Wanawake wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tnanzia (TAWFA) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutembelea Mwalo wa Kibirizi mkoani KIgoma kujionea shughuli zinazofanyika katika Mwalo huo.

Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia Udhibiti Ubora wa Mazao ya Uvuvi na Masoko Bw. Steven Lukanga akieleza jambo alipotembelea na kukagua Mwalo wa Kibirizi mkoani Kigoma mara baada ya uzinduzi wa Mtandao wa Wanawake wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania (TAWFA) Kanda ya Ziwa Tanganyika.

Katibu Mtendaji Kitaifa wa Mtandao wa Wanawake wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania (TAWFA), Bi. Hadija Malibiche akifafanua jambo wakati wa uzinduzi huo.

Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Kitaifa kinachoratibu Muongozo wa Kuendeleza Uvuvi Mdogo nchini (NTT), Bwa. Yahaya Mgawe ( wa pili kulia) akieleza jambo alipotembelea na kuona kazi zinazofanyika katika Mwalo wa Kibirizi mkoani Kigoma.

############

Na Mwandishi wetu- Kigoma

Serikali imesema wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika kusimamia rasilimali za uvuvi pamoja na kuhakikisha biashara ya mazao ya uvuvi inaimarika ndani na nje ya Nchi.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia masuala la Udhibiti Ubora wa Mazao ya Uvuvi na Masoko, Bw. Steven Lukanga kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah wakati akizindua Mtandao wa Wanawake, Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania (TAWFA), Kanda ya Ziwa Tanganyika.

Alisema mchango huo wa wanawake unastahili kupewa thamani kubwa hasa katika kuweka mikakati ya kusimamia changamoto zao ikiwemo kuanzisha Dawati la Jinsia la Uvuvi Wizarani ili shughuli za masuala ya wanawake ziweze kuratibiwa.

“Ninatambua kuwa wanawake wamejiunga katika vikundi mbalimbali ambavyo vinarahisisha utendaji wa shughuli zao za uvuvi na shughuli nyingine katika mnyororo wa thamani, pamoja na hayo vikundi hivi vinakabiliwa na changamoto kama upatikanaji wa masoko, taarifa mbalimbali za bei ambapo shughuli zao zina kuwa ngumu, ”Alisema Bw. Lukanga.

Pia alisema Wizara imeweka juhudi katika kutatua changamoto mbalimbali za wadau wa Sekta ya Uvuvi ili kuongeza mchango wa Sekta kwenye uchumi wa nchi ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara za mazao ya uvuvi, kuzuia uvuvi haramu, kuzuia utoroshwaji holela wa rasilimali za uvuvi, na kuwezesha uvuvi endelevu.

“ Juhudi hizi zinalenga kuwezesha wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi ambao 50% ni wanawake ili waweze kuhimili ushindani wa kibiashara ndani na nje ya nchi na nipende kushukuru Shirika la FAO kupitia Mradi wa Fish4ACP unaotekeleza mradi na kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi katika Ziwa Tanganyika,”alieleza.

Naye Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia uendelezaji wa rasilimali za uvuvi Bi. Merisia Palazo alisema wanawake wote wanaojishughulisha katika mnyororo wa Uvuvi wanatambulika na ndio maana kukawa na jukwaa linalowawezesha kuelezea mambo yao mbalimbali yanayowakabili.

Vilevile Mratibu wa Sekta ya Uvuvi Kitaifa kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Bi. Oliva Mkumbo alisema lengo la kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia uvuvi ili kuinua kipato cha familia na kuondokana na umasikini.

“Kutokana na mchango mkubwa wa kina mama katika shughuli za kiuchumi mradi huo unalenga kumgusa kila mwanamke na kama shirika litaendelea kufungua matawi katika maeneo mbalimbali na hatimaye sekta ya uvuvi kuwa yenye tija,” alifafanua Mratibu huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania (TAWFA), Kitaifa Beatrice Mmbaga alieleza kuwa kuzinduliwa kwa jukwaa hilo ni sehemu ya kutatua changamoto zinazowakabili kina mama katika nyanja ya uvuvi.

MWISHO
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages