Breaking

Monday 18 July 2022

WAZIRI BASHUNGWA ATOA MIEZI MITATU KUKAMILIKA KWA KITUO CHA AFYA KIBONA



OR TAMISEMI - Karagwe


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa ameonesha kutoridhishwa na kasi na viwango vya ujenzi wa Kituo cha Afya Kibona.


Kutokana na hali hiyo, ametoa miezi miwili kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kuhakikisha anasimamia ukamilishaji wa Kituo cha Afya Kibona ili kianze kutoa huduma kwa wananchi.


Waziri Bashungwa ameyasema hayo Julai 18, 2022 wakati wa kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya Kibona kilichopo kata ya Kanoni Wilaya Karagwe.



Alisema hajaridhishwa na kasi na viwango vya ujenzi wa majengo katika kituo hicho.


"Katika taarifa mmeniambia mmefikia asilimia 95 lakini ukiangalia kwa uhalisi sio kweli bado hamjafikia, kwa hiyo natoa miezi miwili kwa ajili ya ukamilishaji ili Serikali ilete vifaa tiba na wananchi waanze kupata huduma," amesema Bashungwa



Amesema tayari Serikali imetoa Sh milioni 500 kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa Kituo cha Afya Kibona ili kiweze kuwahudumia wananchi wa Tarafa ya Kanoni na maeneo ya jirani.


Aidha, Waziri Bashungwa ametoa pongezi kwa wananchi kwa kuendelea kuchangia miradi ya maendeeo ambapo wamechangia Sh milioni 17 na nguvukazi ili kuwezesha ujenzi wa Kituo kituo cha Afya Kibona katika Kata ya Kanoni.


Wakati huo huo, Waziri Bashungwa amemuagiza Meneja wa TARURA Wilaya Karagwe kufanya matengenezo kipande cha barabara kinachoingia kwenye Kituo hicho kuanzia barabara kuu ili iweze kupitika kwa urahisi.


Halmashauri ya Wilaya Karagwe ilipokea Sh milioni 500 kwa awamu mbili kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kibona ambapo awamu ya kwanza walipokea Sh milioni 250 kujenga jengo la wagonjwa wa nje (OPD), maabara na kichomea taka.


Awamu ya pili, Serikali imepeleka Sh milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi na upasuaji, kufulia na njia za watembea kwa miguu kazi iliyoanza kutekelezwa Mei 10 mwaka huu.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages