Breaking

Tuesday 19 July 2022

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YATAJA VIPAUMBELE 7 VYA KUWANUFAISHA WANANCHI 2022/2023




Wizara ya Maliasili na Utalii imeeleza kuwa katika mwaka fedha wa 2022/2023 imejipanga kikamilifu kutekeleza vipaumbele 7 vinavyogusa maisha ya wananchi ili waendelee kunufaika na kazi kubwa inayofanywa na Wizara hiyo ya kuhifadhi, kulinda na kusimamia maliasili na malikale pamoja na kuendeleza utalii nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Mhe. Balozi Dkt Pindi Chana alipokuwa akizungumza na waadishi wa Habari Jijini Dodoma kuelezea vipaumbele vya Wizara yake na mikakati mbalimbali iliyowekwa kuwanufaisha wananchi.

Waziri Balozi Dkt. Chana ameeleza kuwa katika mwaka huu wa fedha, Wizara yake imeindhinishiwa na Bunge kutumia kiasi cha jumla ya Shilingi Bilioni 624,142,732,000 ambazo pamoja na mambo mengine zitatumika katika kutafuta suluhisho la kukabiliana na migongano baina ya binadamu na wanayamapori wakali na waharibifu kupitia utoaji wa elimu, vitendea kazi pamoja na kujenga vituo 19 vya kuwathibiti wanyamapori hao hususan tembo, viboko na mamba kwenye maeneo yenye matukio mengi nchini na kuanzisha matumizi ya mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya kupokea taarifa za matukio hayo hapa nchini.

Sambamba na hilo ameeleza kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi na Wizara nyingine za kisekta ili kuweka mipango bora ya matumizi ya ardhi za vijiji ili kuepusha migongano na hifadhi inayotokana na wananchi kuanzisha makazi katika shoroba ambayo ni maeneo ya mapito ya asili ya wanyamapori.

Aidha, Balozi Dkt. Pindi Chana amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023, Wizara yake imejipanga kikamilifu kuendeleza Programu ya The Royal Tour iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza kasi ya kutangaza utalii kitaifa na kimataifa na kuibua fursa za masoko mapya ya utalii.

Ameongeza kuwa Wizara yake itaendelea kuvitangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii kufikia watalii Bilioni 5 na mapato dola za marekani Bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.

Maeneo mengine ni ukarabati wa miundombinu, kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati, kuimarisha shughuli za upandaji miti, mazao ya misitu na nyuki.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages