Breaking

Friday 19 August 2022

JESHI LA POLISI MWANZA LAJIPANGA KUPUNGUZA AJALI ZA WANAFUNZI



Na Tonny Alphonce, Mwanza

Jeshi la Polisi jijini Mwanza limezindua zoezi maalum la ukaguzi wa Magari yanayobeba wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari Ili Kupunguza ajali zinazoweza kuzuilika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo kamanda wa jeshi la Polisi Mkoani Mwanza Ramadhani Ngh'anzi amesema wameamua kufanya zoezi hilo katika kipindi hiki Cha likizo Ili kutoa nafasi Kwa magari yote kukaguliwa.

Kamanda Ngh'anzi amesema magari yote yanayobeba wanafunzi ambayo yatakuwa hayajakaguliwa katika kipindi hiki Cha zoezi hilo yatakamatwa na kuzuiliwa kutoa huduma hiyo ya kubeba wanafunzi.

"Magari yote yatakayokuwa na dosari tutawapa nafasi wamiliki kwenda kufanya matengenezo na Magari ambayo hayatakuwa na ubovu wowote yatawekewa stika maalum kuonyesha kuwa yanaweza kubeba wanafunzi".alisema kamanda Ngh'anzi.

Aidha kamanda Ngh'anzi amesema jeshi la Polisi Mkoani Mwanza limeandaa kikosi maalum Cha Askari wa usalama barabarani kwaajili ya kutoa elimu Kwa wanafunzi hasa wale wa madarasa ya awali ili waweze kujua matumizi sahihi ya barabara.

"Tutatoa pia semina Kwa shule zote zinazomiki Gari za kubeba wanafunzi,Wahudumu wanaohudumia wanafunzi kwenye Mabasi Ili waweze kujua namna ya kuwasaidia watoto hasa wale wadogo wanapopata changamoto".alisema kamanda Ngh'anzi.

Amesema Askari hao maalum ambao wamepewa mafunzo ya wiki mbili watahakikisha wanafunzi wanajua alama mbalimbali za barabarani ikiwemo namna ya matumizi sahihi ya barabara wakati wote wanapoitumia.

Kamanda Ngh'anzi amesema zoezi hilo litakuwa endelevu na litavigusa vyombo vingine vya moto yakiwemo magari ya abiria,Pikipiki na Magari binafsi nayo yatakaguliwa na kuwekewa stika maalum.

Kwa upande wake dereva wa shule ya Musabe Abdalah Rashidi amesema ukaguzi huo ni mzuri Kwa kuwa unawabana wamiliki kuhakikisha matengenezo ya Magari yanafanyika Kwa wakati.

Nae Mariam Rutachinzibwa mkazi wa Mkolani jijini Mwanza amelitaka jeshi la Polisi kukagua Magari ya shule Kila Siku Ili kudhibiti pia tabia ya baadhi ya shule kujaza wanafunzi wengi kupita kiasi jambo ambalo ni la hatari.

Usalama wa mtoto umekuwa ukisisitizwa kuanzia Mazingira ya Nyumbani hadi Shuleni Kwa lengo la kuhakikisha mtoto anakuwa salama.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages