Breaking

Monday 12 September 2022

ACT WAZALENDO YAITAKA SERIKALI KUSITISHA TOZO, KUTOA UFAFANUZI MAKUSANYO, MATUMIZI



Na Said Muhibu,LLH

Chama cha ACT Wazalendo kimeiomba Serikali kutoa ufafanuzi juu ya makusanyo na matumizi ya fedha zilizopatikana kupitia tozo za miamala ya kielektroniki.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Msemaji wa Sekta ya Fedha na Uchumi wa chama hiko Emmanuel Mvula amesema kuwa Serikali inatakiwa iweke wazi makusanyo ya fedha zote zilizokusanywa tangu kuanzishwa kwa tozo za miamala ya kielektroniki ikwamo ya simu na benki.

"Tunaitaka Serikali kwanza iweke wazi matumizi yote ya fedha zinazotokana na miamala ya simu na benki, watuambie wamekusanya kiasi hiki tozo za benki na kiasi hiki tozo za miamala ya simu," alisema.

Aidha, Mvula amesema kuwa Serikali iweke wazi fedha zipi zilizotumika kujenga vituo vya afya kwani mnamo Septemba mwaka jana Serikali ilipokea fedha za UVIKO-19 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambazo zilitumika kujenga vituo vya afya na kuendeleza miradi mbalimbali Nchini.

"Wakishatuambie walichokusanya, waweke wazi matumizi ya fedha za tozo zilizokusanywa kupitia miamala ya kielektroniki na UVIKO-19," alisema Mvula.

Mnamo Septemba mosi mwaka jana Serikali kupitia Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba ilitoa ufafanuzi juu ya tozo za miamala ya kielektroniki. Dk. Nchemba alisema tozo zimeanzishwa ili kuleta maendeleo kwa watanzania katika kuendesha miradi mbalimbali Nchini.

" Ni tozo, ndiyo, ina maumivu ya hapa na pale, ndiyo na tunatambua kweli kwamba inavuruga ‘purchasing power’ ya mtu mmoja mmoja lakini tuna majukumu ambayo kama nchi na sisi wote kama wazazi tunawajibika kuyabeba kama wajibu wetu,” alisema Dk Mwigulu.

Hata hivyo ACT Wazalendo wameiomba serikali kusitisha tozo hizo na kujifunza kutokana na anguko la miamala yenye thamani ya Trilioni 1.2 kwenye huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi.

Kwa upande mwingine Mvula amemshauri Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum wa makusanyo na matumizi ya fedha zilizopatikana kutokana na tozo ya miamala ya simu na benki hususani katika ujenzi wa vituo vya afya.

"Tunamshauri CAG kufanya ukaguzi maalum, aangalie ubora na thamani ya hivo vituo vya afya pamoja na mapato ya fedha hizo," alisema.

Mvula ameongeza kuwa Serikali isipuuze vilio vya wananchi juu ya tozo hizo huku akisisitiza kuwa zina athari kubwa kuliko malengo yanayotarajia kuvunwa na Serikali.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages