Breaking

Monday 17 October 2022

WAZIRI MCHENGERWA AZINDUA ZOEZI LA KUSAKA NA KUIBUA VIPAJI "MTAA KWA MTAA"Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezindua zoezi la kitaifa la kuibua na kusaka vipaji vya Sanaa la "Mtaa kwa Mtaa" wilayani Rufiji, zoezi ambalo litafanyika nchi nzima.

Uzinduzi huo umefanyika Jumapili Oktoba 16, 2022 katika eneo la Ikwiriri ambapo Waziri Mchengerwa amesema eneo linalofuata baada ya uzinduzi wa huo ni Mkoa wa Arusha ambapo litafanyika kila mtaa ili kuibua vipaji kwenye sanaa.

Amewataka watanzania wenye vipaji vya Sanaa kujitokeza wakati wa zoezi hilo likiendelea ili waweze kuendelezwa baada ya kuibuliwa, huku akisisitiza kauli ya Kipaji chako ndiyo mtaji wako.

"Ndugu zangu hii ni ndoto ya Mheshimiwa Rais wetu, Rais anatamani kuona misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ya kuthamini na kuendeleza Sanaa inaendelezwa ili kuwanufaisha vijana" amesisitiza, Mhe. Mchengerwa

Waziri Mchengerwa Amezitaka mamlaka za wilaya na mikoa kote nchini kusaidia kuibua vipaji vya watanzania ili azma ya Serikali ya kuibua na kuendeleza vipaji vya sanaa iweze kutimia.

Amezihakikishia mamlaka hizo kuwa Wizara ipo tayari wakati wowote kwa wilaya iliyo tayari kuibua vipaji vya Sanaa.

kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Dkt. Kedmon Mapana amesema zoezi hilo limefanyika kwa siku mbili limeibua vipaji vingi ambavyo vinakwenda kuendelezwa.

Katika zoezi hilo ambalo limekuwa na mafanikio makubwa kutokana na wasanii wengi wa Sanaa mbalimbali kujitokeza lilishirikisha viongozi wa Mashirikisho yote ya Sanaa, Baraza la Sanaa kutoka Zanzibar na wadau mbalimbali wa Sanaa.

Akitoa ushuhuda wa hazina ya vipaji vya Sanaa katika Wilaya ya Rufiji mbele ya Mhe. Mchengerwa, Rais aliyewakilisha Shirikisho la Muziki nchini, Mzee Yusufu amesema amefurahishwa na msanii mwenye umri mdogo (11) Musa Mbonde mwenye kipaji kikubwa cha kuimba ambaye amepatia jina la Mzee Yusufu Junior na kuahidi kumsaidia.

Miongoni mwa Sanaa zilizopitiwa ni pamoja na upishi, ngoma, uigizaji, uchongaji na usukaji kwa zaidi ya wasanii 80 katika wilaya ya Rufiji.

Wakisoma risala mbele ya Mhe. Waziri, wasanii wa Wilaya hiyo wamemwomba kupatiwa kituo cha redio, studio na vifaa vya kupigia picha ambapo Mhe. Mchengerwa amesema kuwa atafanyia kazi.

Aidha Waziri Mchengerwa amekagua kazi mbalimbali za Sanaa na kutoa vyeti vya pongezi Kwa wasanii mbalimbali walioibuliwa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages