Breaking

Saturday 29 October 2022

DC MISENYI AWATAKA MADIWANI KUPAMBANA NA TATIZO LA VYOO MASHULENI


Na Lydia Lugakila, Kagera

Mkuu wa wilaya ya Misenyi mkoani Kagera Kanali Wilson Sakulo amewataka madiwani wilayani humo kupambana na changamoto ya vyoo katika shule za msingi na sekondari kutokana na kubaini uwepo wa tatizo la ukosefu wa vyoo.


Kanali Sakulo ametoa kauli hiyo kikao cha baraza la madiwani cha robo ya kwanza (julai-septemba),2022/2023 kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.


Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa amekuwa akitembelea baadhi ya shule za msingi na sekondari wilayani humo na kubaini changamoto ya vyoo jambo linalosababisha wanafunzi kusoma katika mazingira yasiyo rafiki.


"Niwaombe mnapokuwa katika kata zenu na katika majukumu yenu fuatilieni na kutoa hamasa ili kuondoa tatizo la vyoo alisema Kanali Sakulo"


Ameongeza kuwa hadi sasa tayari halmashauri hiyo imefanikiwa kujenga matundu 6 ya vyoo katika shule ya msingi Kyaka.


Aidha amewapongeza madiwani hao kwa jinsi wanavyofuatilia na kusimamia miradi mbalimbali inayoletwa katika halmashauri hiyo.


 Hata hivyo amewahimiza kufuatilia ujenzi wa madarasa 10 yanayojengwa katika kata kumi yamalizike mapema ili kufikia mwaka 2023 pawepo na madarasa ya kutosha na wanafunzi wapate elimu bila kikwazo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages