Breaking

Friday 28 October 2022

MABAKI YA MABOMU VITA YA IDD AMIN KAGERA YALIPUKA NA KUUA, SERIKALI YAOMBWA KUTUMA WATAALAMU KUCHUNGUZA



Na Lydia Lugakila, Kagera

Diwani wa kata ya Nsunga Wilayani Misenyi mkoani Kagera, kupitia kikao cha baraza la madiwani ameiomba serikali kutuma timu ya wataalam watakaochunguza na kuondoa mabaki ya mabomu yanayosadikika kubaki ardhini wakati wa Vita ya Idd Amin baada ya kutokea mlipuko wa bomu na kusababisha kifo cha mwanamme mmoja.

kauli hiyo imetolewa Oktoba 27, 2022 na diwani wa Kata ya Nsunga wilayani humo, Jamal Suleiman, wakati akiwasilisha taarifa utekelezaji wa Shughuliza za maendeleo ya Kata hiyo kwa Kipindi Cha Robo ya kwanza Julai hadi Septemba Mwaka 2022/2023.

Suleiman amesema kuwa ndani ya kata hiyo kumejitokeza matukio mbalimbali likiwemo la Agost 28 mwaka huu la mwanamke aliyejulikana kwa jina Verediana Christopher kupoteza maisha wakati akiendelea na shughuli za kilimo shambani baada ya jembe alilokuwa akitumia kugonga mabaki ya bomu ardhini kisha kulipuka.

Diwani huyo ametumia nafasi hiyo kuiomba serikali kutuma wataalamu ili kuchunguza na kuona namna ya kuondoa tatizo hilo kwani hadi sasa wananchi katika kata ya Nsunga wameendelea kugubikwa na wasi wasi.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya hiyo Kanali Wilson Sakulo amekiri kuwepo kwa mabaki hayo na kuwa tayari wametuma andiko kwa mkuu wa mkoa huo, ili aweze kutuma jeshi la wananchi kitengo cha waandisi wa medani ili waweza kuchunguza na kuondoa mabaki hayo.

"Wananchi nawaombeni mtoe taarifa endapo mtabaini kitu chochote cha chuma ambacho sio cha kawaida"alisema Kanali Sakulo.

Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya ameongeza kuwa hivi karibuni mtu mmoja aliona chuma ambacho sio cha kawaida karibu na nyumba yake na kutoa taarifa ambapo ilibainika kuwa ni bomu,huku akiwasihi kuendelea kuwa wavumilivu.

Ikimbukwe kuwa mnamo Oktoba 1978 Idd Amin alianzisha vita dhidi ya Tanzania kwa kuvamia sehemu za mkoa wa Kagera.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages