Breaking

Tuesday 15 November 2022

AUAWA KWA KUINGILIA UGOMVI WA MUME NA MKEMwanamume mmoja kutoka Gibarori, Kuria Mashariki katika kaunti ya Migori amepoteza maisha baada ya kuawa alipojaribu kuingilia vita vya jirani aliyekuwa akipigana na mke wake.

Ripoti ya polisi inaonyesha kuwa David Chacha mwenye umri wa miaka 32, alikuwa akizozana na mke wake Mary Chacha mwenye umri wa miaka 24, ambaye baadaye alitoroka na kukimbilia nyumbani kwa mama mkwe wake.

Akiwa na hasira za mkizi, David alimfuata mkewe hadi nyumbani kwa mama yake ambapo alimpokeza kichapo zaidi.

Mama yake David, alipiga kamsa ambayo iliwaita majirani ambapo David alimpiga mmoja wa majirani hao na chuma kichwani na kusababisha jeraha kubwa kichwani.

"Polisi walitembelea eneo la tukio na kubaini kuwa David Chacha mwenye umri wa miaka 32, alikuwa na ugomvi wa kinyumbani na mkewe Mary Chacha mwenye umri wa miaka 24.

Mkewe alitorokea kwa mamakwe ambapo David alimfuata na kumpiga zaidi," "Mama mkwe alipiga nduru ambapo jirani Ronald alifika kuwaokoa na kupigwa na chuma kichwani na David," ripoti ya polisi ilisoma kwa sehemu.

Ronald alikimbizwa katika Hospitali ya Mother and Child ambapo alipewa rufaa hadi Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kehancha na baadaye katika Hospitali ya Migori Level 4 ambapo alithibitishwa kufariki alipowasili.

Mshukiwa alikamatwa katika eneo la Motemorabu alikokuwa ametorokea na kulikuwa na taarifa kwamba alikuwa amekimbilia Tanzania.

“Baadaye mshukiwa alitorokea kusikojulikana lakini baadaye alifuatiliwa hadi Motemorabu alikokuwa amejificha,” ripoti ya polisi iliongeza.

Mwili wa marehemu ulihamishiwa na kupelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Hospitali ya Kehancha ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti.
Chanzo: Tuko
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages