Breaking

Wednesday 9 November 2022

GST YAANZA UTEKELEZAJI AGIZO LA DKT.BITEKO KUFANYA UTAFITI WA MADINI MAHENGE



Na.Samwel Mtuwa- Morogoro

Timu ya Wataalam wa Utafiti wa Madini kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania ( GST) imeanza kazi ya Utafiti Katika mkoa wa kimadini Mahenge wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro.

Kuanza kwa utafiti huu ni utekelezaji wa agizo la waziri wa Madini Dkt.Doto Biteko alilolitoa oktoba 29,2022 wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya Mkoa wa kimadini Mahenge.


Katika kuhakikisha utekelezaji wa agizo hilo Mtendaji Mkuu wa GST Dkt.Mussa Budeba akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa amesema kuwa GST itafanya kazi hii ya utafiti kupitia wataalam wake ili kufahamu aina za madini yaliyopo kupitia na matokeo yake yatawasilishwa katika mamlaka husika kwa ajili ya kuvutia wawekezaji ndani ya Mkoa huo.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa ameipongeza GST kwa kuitikia wito kwa wakati na kuonesha ushirikiano mzuri na kusema kuwa viongozi wa mkoa na wilaya watatoa ushirikiano wa kina ili kufanikisha zoezi Zima la utafiti utakaoibua fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya madini ndani na nje ya mkoa huo.

"Binafsi nawapongeza sana kwa kufika hapa Morogoro na kuanza taratibu za kufanya utafiti na nina amini kuwa kukamilika Kwa Utafiti huo kutaleta fursa mbalimbali za uwekezaji ndani na nje ya mkoa wetu wa Morogoro" Fatma alisema.


Awali akizungumza na mkuu wa mkoa Dkt.Budeba alimtaarifu kuwa GST pia imejipanga kutoa mafunzo ya kitaalam kwa wachimbaji wadogo wa madini ili wafanye uchimbaji ulio na tija.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Ulanga katika mkoa wa kimadini Mahenge Ngollo Malenya aliishukuru GST kwa kufika akisema kuwa kukamilika kwa utafiti kutawezesha kujua aina za madini zilizopo na kuwaeleza wadau wa sekta hii na kuwashawishi kuja kuwekeza kwasasa hatuna taarifa ya utafiti wa madini na tunashindwa kuwaeleza wadau juu ya fursa zilizopo.


"Hivyo naamini kuwa kuja kwa GST kutafungua milango mipya katika sekta ya madini hasa katika mkoa huu wa kimadini Mahenge uliozinduliwa hivi karibuni na Waziri Dkt.Doto Biteko"

Sambamba na Utafiti katika mkoa wa kimadini Mahenge GST pia inafanya utafiti kwa wachimbaji wadogo wa Madini katika wilaya ya Gairo mkoani Morogoro wa kujua aina na uelekeo wa miamba katika eneo la Kitaita.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages