Breaking

Sunday 13 November 2022

MIEZI MITATU YA RC CHALAMILA KAGERA, AGUNDUA VIPAUMBELE VYENYE TIJA



Na Lydia Lugakila, Kagera

Mkuu wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila amesema kuwa mkoa wa Kagera umebarikiwa kuwa na Rasilimali ambazo wananchi wake wakizitumia vizuri zinaweza kuleta tija kwao.

Akizungumza na waandishi wa habari RC Chalamila amesema kuwa tangu Julai 28,2022 hadi sasa ametimiza miezi mitatu tangu ateuliwe na Rais Samia kuuongoza Mkoa huo na kuwa baada ya kuujua na kuutambua vizuri amegundua vipaumbele kadhaa vyenye tija vinavyoweza kuufanya mkoa huo kupanda juu zaidi kiuchumi na kuwanufaisha wananchi wake.

Amesema kuwa mkoa wa Kagera wenye watu takribani Milioni mbili na laki tisa umekuwa ukifanya vizuri katika sekta ya kilimo huku matarajio yake yakiwa ni kuliendeleza zao la ndizi na kulifanya kuwa la kibiashara zaidi ambapo tayari maandalizi ya kutuma ujumbe wa wataalam kwenda nje ya nchi zinazolima na kusafirisha ndizi kwa wingi yameanza.

"Ndizi zetu zitaanza kutumwa kitaalam ili kumuokoa mkulima wa kawaida wa zao hilo katika dunia nchi kubwa kwa kusafirisha ndizi kwenda nchi za ulaya ni Jamaica ikifuatiwa na Brazil hivyo tujipange Kisawa sawa alisema Chalamila".

Kwa upande wa zao la kahawa amesema kazi iliyopo kwa sasa ni kuhamasisha zaidi katika uwekezaji katika sekta ya kahawa ili kupandisha thamani ya zao hilo na kuongeza viwanda huku akiwataka wawekezaji zaidi kujitokeza ili zao hilo liwe na tija kubwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Katika sekta ya elimu amempongeza Rais Samia kwa kuboresha sekta hiyo hasa kufuta ada kwa shule za msingi hadi kidato cha sita ili kuruhusu kuwepo kwa shule nyingi.

Aidha ameongeza kuwa mkoa huo umejipanga kila mwaka kufuatilia wanufaika wa bodi ya mikopo wanufaika wa elimu ya juu, ambapo watatakiwa kujua ni wanafunzi wangapi wanufaike kila mwaka hivyo ofisi yake kwa kushirikiana na wabunge lazima wahakikishe wanapambana na suala hilo ambapo tayari Rais Samia ameisha wekeza zaidi Bilioni 400 ili kuhakikisha fedha hizo zinalipa ada ya wanafunzi elimu ya juu.

Hata hivyo katika sekta ya mifugo na uvuvi mkuu huyo wa mkoa amesema watapitia upya lanchi na iligundulika kuna ufugaji wa kawaida usio na tija mkataba utasitishwa kwa haraka ili kuruhusu wawekezaji wenye kuwekeza kiukweli ukweli waanze kazi hiyo ambapo pia ameongeza kuwa uwepo wa ziwa Victoria ni fursa ya kiuchumi na kuwa Rais Samia amekubali wavuvi waanze kupata mikopo isiyo na riba kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya uvuvi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages