Breaking

Wednesday 30 November 2022

WANANCHI TABORA WAPANDA MITI 500 KUOKOA BWAWA LA IGOMBE



Na Lucas Raphael,Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian ameongoza mamia ya wakazi ya Kijiji cha Kigombe, Kata ya Kabila na wadau mbalimbali wa Mkoa huo kupanda miti zaidi ya 500 ili kulinda chanzo cha bwawa la maji la Igombe.

Akizindua kampeni ya upandaji miti kwenye vyanzo vya maji juzi, alisema bwawa hilo lililopo katika manispaa ya Tabora ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya maji katika Mkoa huo ambavyo vimekuwa vikiharibiwa kutokana na shughuli za kibinadamu zinazofanyika kando kando yake.

Alisema uharibifu wa misitu unaoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali kwa kukata miti ovyo unapelekea kuwepo ukame katika maeneo mengi hivyo kukosa mvua za kutosha na kina cha maji kupungua katika mabwawa mengi.

Aliongeza kuwa uharibifu huo pia hupelekea kupungua kwa uzalishaji wa nishati ya umeme katika mabwawa hivyo kuathiri upatikanaji wa huduma hiyo hali inayopelekea huduma hizo kuanza kutolewa kwa mgao.

Balozi Dkt Batilda alisisitiza kuwa kama jamii itazingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi na kufuata maelekezo ya wataalamu tutaepuka athari hizo na kuongeza kuwa hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa kwa wote wanaoenda kinyume.

‘Hatutakubali vitendo hivi viendelee, tumeanza kampeni ya kupanda miti katika vyanzo vyote vya maji na kuanzia sasa tutasimamia kikamilifu sheria zilizopo ili kurejesha mazingira ya vyanzo hivyo katika hali yake ya kawaida’, alisema.

Aidha katika kuhakikisha vyanzo vyote vya maji katika Mkoa huo vinakuwa salama, RC aliagiza Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Mkoani humo kubainisha maeneo yote yenye vyanzo vya maji ili ipandwe miti ya kutosha.

Ili zoezi hilo kuwa endelevu, aliagiza Wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanapanda miti mil 1.5 ambapo zaidi ya miti mil 12 inatarajiwa kupandwa na halmashauri zote 8 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais.

Meneja wa TFS Kanda ya Magharibi Ebrantino Migiye alimshukuru kwa kukubali kuzindua kampeni hiyo na kumhakikishia kuwa wameotesha miche ya miti aina mbalimbali ya kutosha ambayo itapandwa katika maeneo yote ya vyanzo vya maji.

Aliitaka jamii kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita katika suala zima la utunzaji wa mazingira ili kuepusha athari za ukosefu wa mvua na kulinda mazingira yao.

Mwisho.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages