Breaking

Thursday 19 January 2023

SERIKALI YAANZA HATUA ZA AWALI UJENZI MABWAWA NA SKIMU ZA UMWAGILIAJI



Na Wizara ya Kilimo

Kufuatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha Mpaka wa GN. 28, Serikali imeanza kufanya kazi ya kuyapitia maeneo yote ya kilimo kwa lengo la kujenga mabwawa 6 na skimu za kisasa za umwagiliaji ili kuendeleza takribani ekari 91,231 ambazo zitatumika na wakulima kuzalisha mazao yao kwa tija.


Akiwa ziarani Wilayani Mbarali leo tarehe 18 Januari, 2023 Naibu Waziri wa Kilimo, Mh. Anthony Mavunde ametembelea Bwawa la Lwanyo lililopo kata ya Igurusi na Skimu ya Umwagiliaji ya Igumbilo iliyopo Kata ya Chimala,Wilayani Mbarali-Mbeya na kuangalia maeneo ambayo ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya wakulima utafanyika.

"Sisi kama Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba tunajenga miundombinu rafiki ambayo haitaruhusu upotevu wa maji, kumfanya mkulima azalishe mwaka mzima kwa tija na baadaye maji yatayotumika yaweze kutiririka kwenda Mto Ruaha kwa ajili ya shughuli nyingine za kimaendeleo

Kukamilika kwa ujenzi wa miradi hiyo Mbarali kutaenda sambamba na kuwapanga wakulima kwenye mashamba ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za ugani, ili wazalishe kwa tija zaidi na kujiongezea kipato”Alisema Mavunde

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa alieleza kuwa Serikali katika bajeti ya mwaka 2022/2023 imetenga zaidi ya bilioni 83 kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji Wilayani Mbarali ikiwemo ujenzi wa mabwawa na skimu za kisasa na katika mwaka ujao wa fedha serikali itaanza utekelezaji wa miradi hiyo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Mh. Francis Mtega aliishukuru Serikali kwa kuleta miradi mikubwa ya umwagiliaji wilayani Mbarali ambayo inalenga kuwaongezea kipato wana Mbarali na kuchangia zaidi kwenye upatikanaji wa chakula nchini.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Mh. Reuben Mfune alimueleza Naibu Waziri Mavunde kuwa, kilio kikubwa cha wananchi wa Mbarali kimesikika kuhusu kuendeleza skimu za wakulima wadogo zipatazo 88 ili waweze kuzalisha kwa tija.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages