Breaking

Thursday 19 January 2023

USHIRIKIANO WA TANZANIA NA CANADA SEKTA YA MADINI UNAENDELEA KUIMARIKA



Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Canada katika sekta ya Madini umeendelea kuimarika hususan katika masuala ya utafiti wa madini.

Dkt. Biteko ameyabainisha hayo leo Januari 19, 2023 mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Canada nchini Tanzania Mhe. Kyle Nunas Ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma.

Dkt. Biteko amesema baadhi ya maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini nchini Tanzania yaligunduliwa na kampuni za utafiti kutoka nchini Canada hivyo, upo ushirikiano mkubwa kwenye sekta ya Madini kati ya nchi hizo mbili.

Aidha, Dkt. Biteko amemweleza Balozi Nunas kuhusu mabadiliko yaliyofanywa katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 yaliyofanyika Mwaka 2017 likiwemo suala la ufungaji wa migodi, mazingira, na miongozo ya upatikanaji wa leseni za utafiti, leseni za uchimbaji mdogo, wa kati na mkubwa.

Pia, Dkt. Biteko amesema Sheria ya Madini inazitaka kampuni zote za utafiti nchini kutoa taarifa za utafiti kila baada ya miezi mitatu ambapo kushindwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Biteko ametoa wito kwa kampuni kutoka Canada kuwekeza Tanzania hususan katika sekta ya Madini ambapo amesema Kanuni na Miongozo mbalimbali katika sekta ya Madini inamlinda mwekezaji ili anufaike na watanzania wanufaike na uwekezaji huo.

Pia, Dkt. Biteko amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na madini mbalimbali yakiwemo madini ya kimkakati yanayohitajika zaidi kwenye matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo magari yanayotumia nishati ya umeme.

Mazungumzo hayo pia yamemuhusisha Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages