Breaking

Thursday 19 January 2023

MAKAMU WA RAIS AKEMEA TABIA YA WIZI WA MAJI, WANANCHI KUBAMBIKIZIWA BILI



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Philip Mpango amezitaka Mamlaka za Maji pamoja na wadau wengine wa sekta hiyo kuongeza weledi katika usimamizi wa rasilimali za maji kwa kujenga miundombinu mingi zaidi ya kutunza maji na kuvuna maji ya mvua ili kukabiliana na changamoto za maji ambazo hujitokeza.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akiweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria utakaohudumia Tinde na Shelui unaogharimu shilingi bilioni 24.4, hafla iliofanyika eneo la Tinde mkoani Shinyanga leo tarehe 19 Januari 2023.

Amewataka kuongeza ufanisi katika matumizi ya maji, hususan kwenye kilimo pamoja na kuwaagiza kutunza vyanzo vya maji ikiwemo chanzo cha Ziwa Victoria kilichopo Ihelele Wilayani Misungwi, ambacho ni tegemeo kwa upatikanaji wa huduma za maji katika Miji ya Wilaya za Misungwi, Kahama, Shinyanga, Tabora, Kahama, Nzega, Igunga, Shelui na Tinde.

Aidha Dkt. Mpango amesema dhamira ya Serikali ni kuona mradi huo unatoa maji na kuwa endelevu kwa wananchi kama ilivyokusudiwa na pia juhudi za kupeleka maji katika maeneo yaliyopo karibu na mradi huo zinaendelea ikiwa ni pamoja na kuhakikisha maeneo yote yanapata majisafi na salama na yanatosheleza mahitaji.


Makamu wa Rais ameongeza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeamua kutoa kipaumbele cha juu kugharamia miradi ya maji ili itoe huduma endelevu ya majisafi na salama pamoja na elimu ya usafi wa mazingira kwa wananchi wote.

Amesema Sekta hiyo ni miongoni mwa Sekta za kipaumbele katika Mkakati wa kukuza Uchumi wa Viwanda na kupambana na umaskini nchini. Amesema kuboresha huduma ya maji kutapunguza muda wa kutafuta na kuchota maji ili kuwawezesha Wananchi kufanya kazi nyingine za maendeleo,kuongezeka kwa muda wa Wanafunzi kuhudhuria masomo, kuimarisha afya za Wananchi na kuepusha magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.


Halikadhalika Makamu wa Rais amekemea tabia ya wizi wa maji inayofanywa na baadhi ya watu nchini wakiwemo wawekezaji wakubwa.

Amezitaka mamlaka kuacha kutoza faini ndogo kwa wanaokutwa na hatia za wizi wa maji.

Aidha amevitaka vyombo vyote husika kufuatilia na kuwachukulia hatua wezi wote pamoja na wale wanaochepusha maji kutoka kwenye mito bila vibali halali na wengine kuharibu vyanzo vya maji.

Kwa upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema Wizara hiyo inatekeleza miradi ya maji ya kimkakati katika mkoa wa Shinyanga inayogharimu shilingi bilioni 35 itakayosaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa mkoa huo kuondokana na changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama.

Aweso amesema pamoja na wananchi wa kata ya Tinde kunufaika na mradi huo pia vijiji 22 vya Jirani vitaweza kufikiwa na mradi utakaowasaidia wananchi kupata maji safi na salama.

Ameongeza kwamba Wizara hiyo itaendelea kufuatilia na kusimamia kwa makini utekelezwaji wa miradi ya maji ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kutoka huduma kwa wananchi katika kufikia adhma ya kufikisha maji kwa asilimia 95 maeneo ya mijini na asilimia 85 maeneo ya vijijini ifikapo mwaka 2025.

Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Shinyanga.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages