Breaking

Monday 9 January 2023

DKT. KIRUSWA KUSHIRIKI KONGAMANO LA PILI UZALISHAJI MADINI MKAKATI SAUDI ARABIA



Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa anatarajiwa kuiwakilisha Tanzania katika Kongamano la pili la uzalishaji wa Madini mkakati la Wizara za Madini kutoka nchi za Kanda ya Afrika, Mashariki ya Kati na Asia litakalofanyika jijini Riyadh Saudi Arabia.

Kongamano hilo la siku tatu (3) linatarajiwa kuweka msisitizo kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano kati ya Serikali, mataifa na wadau, jambo ambalo ni la msingi kwa maendeleo endelevu ya madini mkakati kwa faida ya jamii husika.

Aidha, kongamano hilo litajadili agenda ya jinsi uzalishaji wa madini ya kimkakati yatakavyoweza kujenga uchumi wa nchi husika pasipo kuchafua mazingira kupitia teknolojia mpya kwa mfano ya utengenezaji magari yanayotumia umeme, betri za kuchaji, na nishati jadidifu.

Vilevile, kongamano hilo linatarajia kujadili agenda kuhusu kuongezeka kwa uhitaji wa madini ya kimkakati duniani na namna ya kushirikiana katika kutumia fursa zilizopo ili madini hayo yazalishwe kwa tija na kwa faida ya nchi husika, raia wake na wawekezaji wa ndani na nje.

Kongamano hilo la pili kuitishwa na Falme ya Saudi Arabia litajadili kwa kina changamoto na fursa zilizopo na wadau wakishirikiana kupitia matumizi ya teknolojia mpya kuzalisha madini ya kimkakati ambazo zitachangia kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi.

Katika kongamano hilo Dkt. Kiruswa amengozana na Wataalam wa Wizara ya Madini kushiriki.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages